ZANINI OTHUMAN, MWANAMKE ANAYEFANYA KAZI ZA NDANI MIAKA 20 KWA BOSI MMOJA
ZANINI OTHUMAN, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti Chama cha Wafanyakazi za Majumbani Mkoa wa Dar es Salaam, alianza kufanya kazi za nyumbani mwaka 2003 baada ya kufiwa na baba yake.
Mara kadhaa kumeripotiwa matukio ya kikatili yanayodaiwa kufanywa na wafanyakazi wa ndani, ikiwamo kuwaua au kuwapiga watoto wa mabosi zao wakati wazazi husika wakiwa hawapo nyumbani, hali ambayo imesababisha kujenga uadui kati ya wafanyakazi wa ndani na waajiri.
Hatua hiyo, imesababisha wenye uwezo kufunga kamera maalumu za kufuatilia matukio yanayoendelea ndani ya nyumba, lengo likiwa kuwalinda watoto wao wasifanyiwe vitendo vibaya na wafanyakazi hao.
Hata hivyo, hali hiyo ni tofauti na mfanyakazi wa ndani, Zanini Othuman kwa kile alichoeleza kuwa upendo uliopo kati yake na watoto wa mwajiri wake ni mkubwa kiasi cha kumsaidia asipoteza kazi yake.
Zanini alipata ujauzito mwaka 2006 na bosi wake alitaka kumwachisha kazi asirejee tena baada ya kujifungua.
"Pamoja na mwajiri wangu kunifanyisha kazi kipindi
chote cha miezi tisa ya mimba, ilipofika muda wa kwenda kujifungua, aliniambia
nisirudi tena na angetafuta mfanyakazi mwingine, ikizingatiwa msichana wake
mwingine aliyeondoka kabla yake alipatwa na changamoto kama hiyo, hivyo akaona
yatakuwa yale yale,” amesema Zanini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama
cha Wafanyakazi za Majumbani, cheo alichokipata mwaka 2018.
"Maamuzi haya ya bosi wangu kuwa nisirudi kazini
yaliniumiza sana, ukizingatia ni kazi niliyokuwa naitegemea inisaidie kumlea na
mtoto wangu, nilimwitikia tu, lakini kiukweli nilikuwa nimeshapoteza mwelekeo
na kutojua nini hasa nitafanya."
Hata hivyo, wakati siku zikiwa zinaelekea ukingoni, Zanini
ambaye anafanya kazi ya kwenda kazini na kulala nyumbani kwake, anasema
aliwaaga watoto wa bosi wake kuwa hatarudi tena akishakwenda kujifungua kwa
kuwa mama yao kakataa asifanye kazi tena.
Kwa kuwa watoto wa bosi wake walikuwa wanampenda kwa jinsi
alivyoishi nao kwa upendo, walimwambia wataongea na mama yao asimwachishe kazi
na kumshauri kipindi ambacho yupo kwenye uzazi ni vema akamtafuta mtu mbadala
wa kumshikia.
"Waliniambia nimtafute mtu ninayemjua ili itakapofika
wakati wa kurejea kazini iwe rahisi kumuondoa, pindi nitakapokuwa tayari
kurudi,” anasema mfanyakazi huyo.
Zanini anasema hilo alilitelekeza, na baada ya kumaliza siku
40 za uzazi alirejea kazini kuendelea na shughuli zake, kazi anayoifanya hadi
leo.
Mama huyo wa watoto wawili kwa sasa anasema, "Nina
imani haya yote yalifanyika kwa kuwa nilikuwa nikiishi vizuri na watoto wa bosi
wangu, kama watoto wameridhika mfanyakazi ni nadra sana kufukuzwa, labda uwe na
matatizo yako mengine na bosi."
Nini kajifunza?
Kutokana na yaliyomkuta katika ajira yake, Zanini anasema
anatamani mkataba wa kimataifa namba 189 wa wafanyakazi majumbani, uridhiwe na
Serikali haraka kwa kuwa pamoja na kuzungumzia haki mbalimbali wanazopaswa
kupewa wafanyakazi, limo suala la likizo.
"Pia naiomba jamii ielewe kwamba mfanyakazi wa ndani
ana haki ya kuanzisha familia yake, na sio inapofika katika hatua hiyo
anaonekana kama mkosaji na kupoteza kibarua chake, kwa ni moja ya kesi nyingi
anazozipokea kutoka kwa wanachama na waajiri wao," anasema Zanini ambaye
baada ya kujifungua mtoto wake alikuwa akimuacha kwa mama yake kisha yeye
anakwenda kazini.
Zanini anaiomba jamii kuwathamini wafanyakazi wa majumbani
kwa kile alichosema ukiwatenda vibaya ni rahisi kudhuru familia, “hawa ndio
walinzi wa nyumba na wapishi.”
Anasema kutowathamini wafanyakazi wa ndani ni chanzo cha
kufanya ukatili dhidi ya mabosi au watoto wa mabosi wao.
Changamoto kama hizo, anasema huwa anakutana nazo kwa
wanachama wake, lakini yeye aliponea kwa watoto wa bosi wake kwa kuwa walikuwa
wanampenda.
“Wito wangu kwa jamii kuwaona wafanyakazi wa ndani nao wana
mahitaji yao, na huwa wana haki ya kuwa na familia pia, hivyo inapotokea
mfanyakazi kapata ujauzito apewe likizo ya uzazi kama ilivyo kwa wafanyakazi
wengine.”
Anafanyaje kazi za chama
Zanini anasema yeye akiwa mwenyekiti wa wafanyakazi wa ndani
anashukuru anapata muda pia wa kufanya kazi za chama kwa kuwa bosi wake amekuwa
akimuunga mkono katika hilo.
"Nashukuru bosi anajua mimi ni mwenyekiti katika chama
changu, ananipa muda wa kufanya kazi za kichama, kikubwa tu niwe nimemaliza
kutekeleza majukumu yangu na hata ikitokea napaswa kusafiri huwa nikimpa
taarifa mapema," anasema Zanini.
Akieleza changamoto anazozipata katika kuongoza chama hicho, anasema kuna ugumu wa kuwapata wanachama, hasa wanaoishi kwa mwajiri, hivyo anachofanya ni kuwavizia wakiwa wanaenda dukani au kuwasindikiza watoto kupanda gari la shule, njia zinazotumiwa pia na viongozi wa mikoani.
Zanini anasema kuwa anawatambua kama ni wafanyakazi wa ndani kwa kuwaangalia kwani wanajuana, hasa maeneo ya Upanga, wengi wanavalishwa sare siku hizi.
Mpaka sasa chama hicho kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuna
wanachama 30, huku Taifa wakiwa 5,000, lakini malengo kufikia 10,000 mwaka
2025.
“Ili kuongeza wanachama kirahisi, naomba maofisa kazi
wanisaidie kuwafikia wafanyakazi wengine wa ndani kwa kuwa anaamini asilimia
kubwa nyumba zina wafanyakazi hao,” anasema Zanini.
Mikataba ya wafanyakazi wa ndani
Mwanasheria wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani Hifadhi,
Hotelini, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu), Wagala Shungu, anaungana na
Zanini na kueleza alichofanyiwa mfanyakazi huyo ndio wengi hufanyiwa na
kuwataka waajiri kuzingatia mikataba ya kazi.
Wagala anasema hayo yote ni matokea ya waajiri na
wafanyakazi kuingia mikataba ya mdomo licha ya Serikali katika sheria za kazi
inataka waingie mikataba ya kimaandishi.
Anasema haki hizo za likizo ya uzazi zipo, lakini hakuna
ufuatiliaji na wafanyakazi wenyewe hawajui kama wana haki hizo.
Kutokana na hilo, mwanasheria huyo anasema kwa sasa wamekuwa
wakiupambania mkataba namba 189 wa wafanyakazi kazi za ndani.
Wagala anasema mkataba huo unasisitiza umuhimu wa kuingia
mkataba wa kimaandishi, kupewa haki zote kama wafanyakazi ikiwamo likizo ya
uzazi, mapumziko kwa saa 24, kujiunga na mifuko ya hifadhi za jamii na haki ya
faragha kwa mfanyakazi kuwa na chumba chake mwenyewe cha kuishi.
"Juhudi nyingine tunazozifanya ni kuhakikisha kazi hii
inaheshimiwa, ikiwamo kuja na mtalaa maalumu kwa ajili ya kazi hizo utakaokuwa
ukifundishwa katika vyuo vya ufundi Veta, kazi ambayo tumeifanya kwa
kushirikiana na jumuiya ya watu wanaojitolea ulimwenguni (CVM) Tanzania,”
anasema Wagala.
Anasema programu hiyo ya kuwasomesha wafanyakazi wa
majumbani ina lengo la kuwasaidia kuongeza ujuzi katika kazi zao na kuuzika
kitaifa na kimataifa.
Mratibu wa mradi huo, Ibrahim Mtoni, anasema mradi uliopewa
jina la mradi wa kukuza kazi zenye heshima, haki na utu kwa wafanyakazi wa
majumbani, umekuja wakiamini kutawaongezea uelewa na ufanisi wafanyakazi hao na
kuweza kuuzika kitaifa na kimataifa.
Katika kuteleza hilo, Mtoni anasema wametenga Sh87 milioni
kwa ajili ya kuwasomesha wafanyakazi hao na Sh98 milioni kwa ajili ya kununulia
vifaa mbalimbali kwenye Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta).
“Mradi huu utakuwa na msaada kwa wafanyakazi hawa, kwani
tumekuwa tukishuhudia baadhi yao wakiwa wanafika maeneo yao ya kazi hawana
wanalolijua na mwisho wa siku kuishia kufukuzwa, huku kwa wale wa nje wakiishia
kupewa kazi ambazo sizo walizokwenda kuzifuata,” anasema Mtoni.
Mkuu wa Idara ya Sheria Chodawu, Asteria Mathias, anasema
ili mfanyakazi kuweza kupata mafunzo haya, ni lazima awe mwanachama wa Chodawu
na ada italipwa na chama hicho, baadaye atakatwa kidogokidogo kwenye mshahara
wake, kiasi kisichozidi Sh5,000 kwa mwezi.
Asteria anasema ni lazima mwajiri wake awe ameridhia kwa
maandishi kwa kuwa lazima itamchukulia muda, hasa anapokuwa darasani na kuacha
kazi, “lakini lazima akubali kutoa fedha iliyotumika kumsomesha mfanyakazi wake
katika mshahara atakaomlipa.”
Katika kusoma huko, anasema kuna machaguo mawili, ikiwamo
kusoma kutwa au kulala huko huko, mafunzo yatakayochukua mwezi mmoja na
kuvitaja vyuo vitakavyohusika katika utoaji mafunzo hayo kwa sasa kuwa ni Veta
ya Dodoma, Mikumi Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na VTA Zanzibar.
VETA wanasemaje?
Kwa mujibu wa Veta, wataanza mafunzo hayo Oktoba mwaka huu,
licha ya kuwa walishaanza kwa majaribio, huku wanachama 44 wa Chodawu
wakifaidika.
Ofisa Ukuzaji Mitalaa Veta, Anna Nyoni anasema wameandaa
mitalaa miwili tofauti kati ya hiyo, ipo ya wafanyakazi wa majumbani hapa
nchini na upo wa wafanyakazi wa majumbani wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.
Ndani ya mitalaa hiyo, Anna anasema watajifunza mambo mbalimbali, ikiwamo
mikataba, namna ya kutunza nyumba, kulea watoto na kulea wazee.
Post a Comment