DC KILAKALA APIGA MARUFUKU WANANCHI KUJENGA BILA KIBALI CHA UJENZI NA KUSISITIZA WANANCHI KULIPA KODI YA ARDHI
MKUU wa Wilaya ya Morogoro,Mhe.Mussa Kilakala, amepiga marufuku wananchi kujenga ujenzi holela ambao haufuati taratibu za vibali vya ujenzi.
Agizo hilo amelitoa katika kuadhimisha Wiki ya ardhi iliyofanyika Manispaa ya Morogoro eneo la Ofisi ya ardhi Stendi mpya ya daladala Mafiga Februari 24-2025.
Aidha, DC Kilakala, amesema serikali haina mpango wa kubomoa nyumba za wananchi isipokuwa wanatakiwa kujenga kwa kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha ujenzi.
“Mtu yeyote anayejenga mjini mahali popote bila kufuata utaratibu wa kumilikishwa yaani kiwanja ambacho hakijapimwa, hujamilikishwa, huna kibali cha wenye mamlaka ya mji unaohusika ujue unajipeleka kwenye hatari ya kuvunjiwa na kuondolewa jengo lake" Amesema DC Kilakala.
Hata hivyo,amewataka mafundi wanaojenga nyumba kuhakikisha kabla ya kujenga wanapatiwa kibali cha ujenzi na mwenye eneo ili asiwe kwenye hatari ya kukamatwa yeye pamoja na mwenye eneo la ujenzi.
Pia,amesisitiza suala la ulipaji wa kodi za ardhi,ambapo amesema kodi hizo ndio zinazosaidia Serikali kuboresha huduma ikiwemo miundombinu,ununuzi wa dawa na huduma zote za Kijamiia mabzo Serikali imekuwa ikizifanya kwa wananchi.
Aidha, amepongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kupunguza migogoro ya ardhi nchini hususani Mkoa wa Morogoro kwani kwa sasa migogoro imepungua kwa kiasi kikubwa.
DC Kilakala,amechukua nafasi ya kuwaalika wananchi wa Morogoro katika Kliniki ya ardhi awamu ya nne itakayofanyika Februari 26 hadi Machi 1-2025 katika Ofisi ya ardhi Mafiga.
Kwa upande wake Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Mussa Kayela, amesema ili kurahisisha zoezi la upimaji na utoaji wa hati za viwanja, ni muhimu wananchi kuepuka migogoro ya ardhi, huku akisisitiza suala la Wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya ardhi kwa kutokufanya kitu chochote kwenye ardhi kinachoweza kuwa kero kwa wengine.
Aidha Kamishina Kayela,amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa bilioni 1 kwa ajili ya kupima viwanja eneo la Kiegea na kuwapa wananchi viwanja 1320 bure kutatua changamoto zao za muda mrefu.
Pia ,amemshukuru Rais Samia,kwa kutatua mgogoro mkubwa wa CCT ambao kwa sasa ni Suluhu New City ambapo kwa upendo wake amemega hekari 5113 kuwapatia wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wa Msimamizi wa Sekta ya ardhi Manispaa ya Morogoro, Emiline Kihunrwa,amesema wiki ya ardhi itaambatana na Kliniki ya ardhi yenye lengo la kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa pamoja na kuhamasisha wananchi kulipa kodi ya ardhi.
Kihunrwa,amesema kliniki zote walizozifanya zimekuwa na mafanikio makubwa kwani zaidi ya wananchi 2000 wametaturiwa kero zao.
Kliniki ya Ardhi inatarajiwa kuwa na wataalam wote wa sekta ya Ardhi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro na wa Manispaa ya Morogoro ili kupokea, kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
Post a Comment