MBUNGE ABOOD ATETA NA MABALOZI NA WENYEVITI WA MITAA,AWATAKA WAKAIMARISHE MAHUSIANO KATIKA KUWATUMIKIA WANANCHI WAO
WENYEVITI wa Serikali za Mitaa na Mabalozi Jimbo la Morogoro Mjini wametakiwa kushirikiana kutatua kero za wananchi ili kutekeleza shughuli za miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaaziz Abood,Januari 13-2025 kwenye Ukumbi wa Tanzanite, wakati akizungumza na Wenyeviti wa Mitaa na Mabalozi wa CCM akifunga semina elekezi kwa viongozi hao yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi.
Mh.Abood,ambaye ndiye aliyeandaa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Ofisi ya CCM Wilaya pamoja na kuwaalika wataalamu mbalimbali wa Serikali,amesema semina hiyo ni muhimu kwani itapunguza sana ukiukwaji wa sheria wa kanuni za uongozi zinazopelekea mwingiliano wa majukumu baina ya wenyeviti wa Mitaa na Maafisa Watendaji wa Mitaa yao hali inayopelekea migogoro na kuzorotesha maendeleo.
Aidha, Mh. Abood, amewasisitiza viongozi hao kusimamia vyema miradi ya maendeleo iliyopo katika maeneo yao ili iweze kukamilika kwa ubora uliokusudiwa.
Hata hivyo,Mhe. Abood, amewataka Mabalozi na Wenyeviti kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuboresha huduma kwa wananchi wanaowatumikia na kuweza kutimiza adhma Kuu ya CCM ya kuwa Chama chenye misingi imara na bora na Chama kisichotetereka.
"Mabalozi ndio kiunganishi kikubwa baina ya wananchi na viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maana ya kujua changamoto zao kabla ya kuziwasilisha kwa Wenyeviti wao, hivyo nendeni mkaimarishe uhusiano wenu ili mkatimize na kutekeleza vyema Ilani ya CCM , msiende kurumbana nyie mnatoka nyumba moja, " Amesema Mh. Abood.
Pia,amesema ushirikiano wa Wenyeviti na Mabalozi kwa miaka iliyopita imesaidia Ofisi yake kuweza kuwahudumia zaidi ya wananchi 69000 waliokuwa wanafika Ofisini kwake, hivyo kwa hali hiyo kama ushirikiano ukiimarishwa kutasaidia kuongeza idadi kubwa ya wananchi ambao watakuwa wakihudumiwa katika Ofisi yake lakini kuanzia kwenye ngazi ya Shina, Tawi, Mitaa pamoja na Kata kwa ujumla.
Mbali na mafunzo hayo, Mh.Abood,amesema katika kipindi chake cha miaka 4 inayokwenda miaka 5 sasa yapo mambo mbalimbali ameyafanya katika kuhakikisha anawatumikia wananchi wa Jimbo la Morogoro Mjini ikiwemo huduma za afya,miradi ya shule, miundombinu ya barabara,uwezeshaji kiuchumi n.k.
Hata hivyo,amewaeleza wenyeviti wa Mitaa na Mabalozi kuwa wanayo kila sababu ya kutembea kifua mbele kwani miradi mingi iliyoibuliwa na wananchi kutoka kwenye mitaa yao ikiwemo miradi ya afya,umeme, maji,elimu, miundombinu pamoja na shughuli za uwezeshaji wa kiuchumi imetekelezwa kikamilifu na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye Waziri wa Ujenzi ,Mh. Abdallah Ulega, akitoa salamu zake kwa wajumbe hao baada ya kualikwa kwenye mafunzo hayo, amewahakikishia wananchi kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kwa dhati kuwatumikia wananchi wa Tanzania hususani wananchi wa Jimbo la Morogoro Mjini jambo ambalo limemsukuma Dkt. Samia kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 50 kwa jili ya ujenzi wa barabara ya Kihonda SGR pamoja na kurekebisha madaraja na Barabara zilizoharibiwa na mvua za Elninyo.
Kwa upande wa Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini,Ndug. Twalib Bellege, amesema Chama kitaendelea kusimamia Ilani ya CCM katika kuhakikisha malengo yote ya CCM yanayotokana na Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 yanatimia.
Aidha, Bellege, amempongeza Mh. Abood kwa kuandaa mafunzi hayo kwani anaamini mafunzo hayo yataleta tija katika kusimamia shughuli za maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.
Bellege,amesema kwa Mabalozi na Wenyeviti kuwa Chama hakitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa kiongozi yeyote wa Mtaa ambaye atabainika kwamba hawatendei haki wananchi waliompa dhamana ya kuwatumikia kupitia CCM na hatua hiyo ni kumsimamisha uongozi kwamba hatoshi kuwatumikia wananchi wa eneo husika.
Post a Comment