WAZIRI JAFO AIPONGEZA KANDA YA MASHARIKI, AWATAKA WANANCHI KUTUNZA MAZINGIRA.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (Mb) ameyapongeza maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki kwa maandalizi mazuri huku akitoa wito kwa wananchi kutunza mazingira ili kuepukana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yanaathiri sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.
Waziri Jafo ametoa wito huo Agosti 8 mwaka huu wakati akizungumza na waandaishi wa habari baada ya ziara yake ya siku moja ya kutembelea mabanda na vipando vya maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki vilivyopo eneo la Nanenane katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro maonesho yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Manispaa hiyo.
Waziri huyo amesema, ameridhishwa na maandalizi ya maonesho hayo kutokana na wadau wa sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kuwa wamejiandaa vizuri katika kutoa elimu kwa wakulima ili iwasaidie, kwani kwa kufanya hivyo wametafsiri maelekezo ya Rais Samia ya kuwawezesha wakulima kielimu, zana na pamoja na fedha.
“...binafsi nimefarijika sana na maandalizi mazuri ya maonesho ya wakulima ya mwaka huu katika kanda hii...kwahiyo nimeona kwamba mmeendelea kuwa vinara wa maonesho mazuri ya Nanenane hapa Tanzania...” amesema Waziri Jafo.
Pamoja na pongezi hizo Mhe. Jafo bado amesisitiza suala zima la utunzaji mazingira kwa kuwa amesema kwa sehemu kubwa kilimo kinategemea mvua na kwamba uharibifu wa mazingira unasababisha athari mbalimbali ikiwemo ukame.
Amesema, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi Bil. 214 kwa ajili ya kujenga marambo makubwa 114 hapa nchini kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na bila utunzaji wa mazingira kilimo hicho hakitafanikiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema Kanda ya Mashariki inajukumu la kulinda mazingira kutokana na umuhimu wa mito inayopeleka maji katika bwawa la kufua umeme la Mwl. Nyerere linalotarajia kuzalisha umeme zaidi ya Megawati 2000.
Naye Bw. Said Godfrey kutoka Halmashauri ya ya Wilaya ya Kisarawe Mkoani pwani, amewaeleza wananchi faida ya zao la mchikichi na kubainisha kuwa, koli moja la mchikichi unaweza kutoa lita tano za mafuta na mche huo mmoja unaweza kuzaa makoli zaidi ya 20 kwa mwaka, hivyo ameshauri wananchi wengine kujikita katika kilimo cha zao hilo la michikichi.
Post a Comment