Header Ads

DAKIKA 50 ZA KUFA KUPONA, LORI LA MAFUTA LAANGUKA

DAKIKA 50 zimetajwa kuwatesa wafanyabiashara na wakazi wa Kibo wilayani Ubungo, baada ya lori la mafuta kuanguka katika mtaro na kuwaka moto kabla ya Jeshi la Zimamoto kufika eneo hilo kwa ajili ya uokozi.

Mashuhuda wa ajali hiyo wanasema moto huo ulianza mida ya saa 5 asubuhi baada ya lori hilo lililokuwa limebeba mafuta kuelekea Bukoba mkoani Kagera kuanguka mita chache kutoka katika kituo cha mabasi yaendayo haraka mara baada ya kudaiwa kumkwepa dereva bodaboda.

Hata hivyo, katika dakika 50 za awali ni wakazi wa eneo hilo pekee ndio walikuwa wanashiriki katika uokoaji, huku baada ya muda kidogo Zimamoto walifika na kukabiliana na moto huo kwa takribani saa moja kabla ya kuudhibiti.

Hatimaye, saa 7.32 moto huo ulidhibitiwa na kuzimika kabisa huku baadhi ya mali za karibu na barabara zikiwa zimeharibika.

Mali zilizopo katika maduka ya pembezoni mwa barabara hiyo zimeharibika kutokana na moto wa mafuta uliokuwa ukiwaka na kusambaa hewani na hivyo kuwafanya wakazi wa eneo hilo kuyakimbia makazi yao kwa muda.

"Wakati ajali inatokea tulisikia kishindo kikubwa, tulikuwa ndani. Ilibidi tutoke na hapo tukaona moto umeanza dereva alishuka haraka, akakimbia moto ukaanza kuongezeka kasi na baada ya dakika 15 akatoka kondakta tayari moto umeshika kwenye nguo.

"Dakika tano baadae moto uliripuka ilibidi tukimbie bondeni huko moto ulikuwa mkubwa sana ukitanda barabara zote mbili," amesimulia Monica Japhet mkazi wa Kimara, Kibo.

Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo wamesema wamepoteza mali zao kutoka na athari zilizotokea katika moto huo.

"Mafriji, bidhaa zimeyeyuka kama unavyoona 'anaonyesha' ni hasara kubwa hakuna kinachofaa joto kali limeharibu kabisa bidhaa, moto umewaka kwa dakika zaidi ya 50 ndipo Zimamoto wakafika hapa na wameuzima kwa takribani saa moja unusu ndipo sasa tukaanza kusogea barabarani wote tulikimbilia huko chini," amesema Blessed Ngowi.

Mwendesha Bajaji eneo hilo Frank Kibiki amesema walifanikiwa kumchukua dereva na kondakta wake na kuwawahisha Hospitali ya Temeke kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kamanda wa Zimamoto Kinondoni, Elisha Mugisha amesema wamefanikiwa kuudhibiti moto huo kwa sasa na wanatarajia kuendelea kuwa karibu ili kuondoa madhara yanayoweza kujitokeza.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.