Header Ads

MRADI WA KUSAIDIA KUTABIRI MAGONJWA YA MLIPUKO KWA KUTUMIA MIFUMO YA AKILI MNEMBO WAZINDULIWA MANISPAA YA MOROGORO


HALMASHAURI ya Manispaa ya Mororgoro imezindua mradi wa ukusanyaji taarifa (data) zitakazotumika   kwa ajili ya kutabiri magonjwa ya mlipuko yanayoambukizwa kwa njia ya maji kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia Akili Mnembo (Artificial Intelligence).

Mradi huu unatekelezwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza katika utambulisho wa mradi, Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro ,Ally Machela, amesema amefurahishwa  kuona watafiti wakienda  kwenye maeneo yenye changamoto na kuwekeza katika maeneo yote ili waone hali halisi. 

"Utafiti huu utasaidia kupata data kwa ajili ya mambo mbalimbali ya kiafya, tunawashukuru sana Watafiti wetu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) kwa kuja na mfumo mzuri wenye tija katika Halmshauri yetu ya Morogoro " Amesema Machela.

Kwa upande wa Msimamizi wa mradi  kutoka SUA, Dkt. Neema Lyimo, amesema kuwa mradi huo utakuwa ni suluhisho la kupata data za visababishi vya magonjwa ya mlipuko yanayoambukizwa kwa njia ya maji kama vile homa ya matumbo (typhoid), amoeba na kuharisha, na kutumia akili mnembo kutabiri uwezekano wa mlipuko wa magonjwa hayo yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt. Lyimo, amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na milipuko ya magonjwa mbalimbali, hivyo ukusanyaji huo wa taarifa na mfumo wa  akili mnembo  utasaidia upatikanaji wa taarifa kamili  ya magonjwa hayo,  hivyo kuwezesha mamlaka husika kujiandaa na kuchukua hatua za kudhibiti au kutoa  taarifa za awali za mapema iwezekanavyo  kwa wananchi wake kabla ya mlipuko kutokea. 

''Nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi hivyo kama wataalamu kwa kushirikiana na watafiti wenzangu tuliona umuhimu wake na kupendekeza  utafiti wa kukusanya taarifa juu ya magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na vimelea vya kwenye maji, hasa wakati huu wa mabadiliko ya tabianchi'' Amesema Dkt. Lyimo.

Watafiti wengine kutoka SUA wanaotekeleza  mradi huo ni  wa Akili Mnembo ni Dkt. Silvia Materu, Dkt. Joseph Telemala na Dkt. Kadeghe Fue. Mshiriki mwingine ni  Dr. Ndimile Kilatu kutoka Manispaa ya Morogoro. 

Utambulisho wa mradi  huu umehudhuriwa na Dr. Charles Mkumbachepa (Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro) , Martin Mzuwanda (Kaimu Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro)  na Hezron Ligala (Mratibu wa mfumo wa taarifa za Kinga -NISMIS kutoka Manispaa ya Morogoro).

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.