Header Ads

WAOKOLEWA WAKIWA WAMEFUKIWA NA KIFUSI SIKU 9 GEITA

 WACHIMBAJI wadogo wawili Mpina Shukuru (29) mkazi wa Mganza, wilayani Chato na Renatus Nyanga (35), mkazi wa Sengerema mkoani Mwanza, wameokolewa hai baada ya kufukiwa na kifusi siku tisa, katika mgodi wa Igalula wilayani Nyangwale.

Wachimbaji hao walifukiwa na kifusi usiku wa Agosti mosi, 2023; wameokolewa Agosti 11 huku wakiwa wamedhoofika na kupatiwa huduma ya kwanza na madaktari waliokuwa eneo la tukio, kisha kupelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale kwa matibabu zaidi.

Mganga Mfawidhi wa hiyo, Princepius Mugishagwe, amesema siku ya alhamisi Agosti 10, 2023 saa 2:30 usiku, walipokea taarifa ya wachimbaji kufukiwa na kifufi, ambapo timu ya dharura ya hospitali hiyo ilifika kutoa msaada ambapo tayari walikuwa wametolewa kwenye kifusi.

“Tuliwakuta wana hali mbaya, walikua na shida ya kupumua na kwa kuwa walinasa kwenye kifusi muda mrefu, kiwango cha sukari kilikuwa kimeshuka. Tuliwapa huduma ya kwanza ya dharura na baada ya kujiridhisha tuliwaweka kwenye gari ya wagonjwa na wakaendelea na matibabu hadi saa sita usiku waliweza kuzungumza,” amesema Mugishagwe

Amesema afya zao zinaendelea vizuri lakini mmoja wao vidole vyake vilipata majeraha na wanaendelea na matibabu na wanaweza kuruhusiwa muda wowote maada ya afya zao kutengemaa.

Akizungumza akiwa hospitalini hapo, Shukuru; amesema kuwa siku ya tukio waliingia kwenye shimo saa 12 jioni; kwa ajili ya kufanya kazi na ilipofika saa 7.45 usiku wa kuamkia jumatano wakiwa wanavuta mawe wakiwa watatu duara lilianza kudondosha udongo.

Hata hivyo kwa imeelzwa kuwa baada ya kifusi kuanza kuporomoka mchimbaji mmoja kati ya watatu waliokuwa shimoni alifanikiwa kutoka kabla ya gogo la mti kushuka na kumgonga Mpina kisha kufunga njia.

Shukuru amesema kutokana na njaa na kiu walianza kunywa mkojo wao wenyewe ambapo siku ya jumatatu walisikia tena watu wakigonga na kupata matumaini upya jambo lililomfanya achukue nyundo na kugonga chuma ili waokoaji wapate taarifa.

“Walitufikia wakawa wanatusemesha sisi tumelegea mwili hauna maji tukawaomba maji lakini kila tunapoomba wanasema wanaleta lakini hawakutupa maji hadi tulivyookolewa tukapandishwa juu tulipofika tukapewa maji ndio mwili ukaanza kupata nguvu,” amesema Shukuru.

Mchimbaji mwingine Renatus Nyanga, amesema kuwa njaa na kiu ndio ilikuwa changamoto kubwa kwao na alikata tamaa na kubaki kumuomba Mungu awalinde hadi watoke salama,” nilimuita sana Mungu na roho Mtakatifu na nilimwambia Mungu kama aliniumba kwa udongo huu basi akinitoa salama nitamtumikia nitakua mwinjilisti,” amesema Nyanga.

“Mimi nilikua salama mwenzangu ndio vidole viwili vilivunjika kimoja kilikua kimenin’ginia nikachukua kisu nikakitoa kimoja ndio tuliokiacha mana kilionekana kama kinaweza kupona tulijitahidi kujiokoa wenyewe lakini kila ukijiokoa mawe na matimba yanakurudisha maombi yametusaidia sana,” amesema Nyanga.

Naye Francis Misungwi, ambaye ni baba yake Mpina amesema alipata taarifa ya kufukiwa kwa mtoto wake Agost 2, 2023 na baada ya siku tatu alikata tamaa ya kumpata mwanae akiwa hai na hata familia ilikua tayari imekaa ikisubiri mwili wazike.

Kwa upande wake Hussein Makubi, mmiliki wa leseni ya uchumbaji amesema kazi ya uokozi ilianza Agosti 2, 2023 baada ya kupata taarifa kutoka kwa mmoja wao aliyeokolewa na kusema hawakutegemea kuwakuta hai kwa kuwa kwenye shimo hakukuwa na chakula wala maji.

 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.