Header Ads

SABABU 10 SIMBA KUBEBA UBINGWA


KOCHA wa Simba, Robert Oliveira ‘Robertinho’ amepanga kutumia mbinu ya aliyekuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ya kutoa nafasi ya kucheza kwa kundi kubwa la wachezaji, huku akianika sababu za kwanini kikosi chake kitatwaa ubingwa msimu huu.

Miongoni mwa sababu zilitolewa na Robertinho ni pamoja na kuwa na nyota wenye ubora kila eneo, benchi bora la ufundi, ubora wa kambi ya Uturuki, viongozi kufanya usajili makini na ushirikiano wanaopata kutoka kwao.

Akizungumza baada ya kuwasili nchini tarehe 03 Agosti 2023, Robertinho amesema tofauti na msimu uliopita, awamu hii ana kundi kubwa la wachezaji ambao hawapishani sana viwango, jambo linalompa nguvu ya kusaka ubingwa.

"Kwa sasa tuna uwiano mzuri wa kikosi. Kuna wachezaji wapya wenye ubora wa juu, ni jambo la muhimu na napongeza uongozi. Tuna wigo mpana wa kufanya mabadiliko kama unavyofahamu kuna suala la majeraha na pia mabadiliko ya kimfumo", amesema Robertinho.

"Kiwango ambacho kimeonyeshwa na wachezaji kwenye kambi ya maandalizi ni kizuri na kinafurahisha. Tunaweza kutumia wachezaji tofauti tofauti kwenye nafasi mbalimbali kwa vile wana kiwango kinachofanana" amezungumza kocha.

"Kwa mfano nikitaka kucheza kwa kushambulia sitopanga idadi kubwa ya viungo wa ulinzi, lakini tukiwa na mpango wa kulinda maana yake nina namba ya kutosha ya viungo wa ulinzi," amesema Robertinho.

Kocha huyo amesema kazi kubwa ambayo wameifanya katika kambi ya Uturuki ni kutengeneza uhusiano mzuri wa wachezaji ndani na nje ya uwanja, wakiamini utakuwa ni chachu kwao kufanya vyema.

"Tunahitaji kutimiza malengo ya kufanya vizuri msimu ujao kwa kutwaa ubingwa. Tunahitajika kuwa na timu nzuri na kabla hujawa nayo, unapaswa kuifanya iwe familia na ndicho ambacho tumekifanya. Sasa tuna makundi mawili (timu), ambayo yote tunaweza kuyatumia. Kumbuka tuna mashindano muhimu mengi mbele. Tuna tamasha la Simba Day, ambayo yote tumeweka malengo ya kufanya vizuri. Kuhusu nani atacheza itategemea na ufanisi na mchango wa kila mmoja ndani ya uwanja," amesema Robertinho.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.