Header Ads

BALOZI WA MAZINGIRA AKUTANA NA MAAFISA MAZINGIRA MANISPAA YA MOROGORO KUJADILI HALI YA USAFI WA MJI NA UTUNZAJI VYANZO VYA MAJI.


BALOZI wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Chage Alex Chage, amekutana na Uongozi wa Kitengo cha Mazingira na uhifadhi wa misitu Manispaa ya Morogoro kujadili suala la mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Kikao kazi hicho kimefanyika Agosti 17/2023 katika Ofisi ya Mazingira Manispaa ya Morogoro iliyopo Yadi Magereza.

Akizungumza katika kikao hicho, Chage,amewashukuru Maafisa Mazingira wote nchini kwa kazi kubwa wanayoifanya pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Amesema upo umuhimu  mkubwa sana katika kutunza mazingira unaotokana na vyanzo vya maji katika jamii yetu na nchi kwa ujumla , kama vyanzo hivyo vikitunzwa ipasavyo.

Chage ,amesema licha ya kuwepo na Sheria za Usimamizi wa vyanzo vya maji (bahari, maziwa, mito, mabwawa, na chemichemi) kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji kutokana na kuwepo kwa shughuli za binadamu zinazofanyika pasipo kiuzingatia Sheria zinazosimamia mazingira na rasilimali maji.

Hivyo,amewaomba wananchi kutunza vyanzo hivyo vya maji pamoja na kutotupa takataka katika mifereji na mito inayowazunguka.

Amesema kuwa Tarehe 26/8/2023 watakuwa na Kampeni kubwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mazingira ya Manispaa ya Morogoro katika kufanya usafi Mto Kilakala unaopitia katika Kata ya Kilakala na Boma na kuwaomba Viongozi wa Serikali, Chama na Wananchi kujitokeza kwa wingi.

Naye Mkuu wa Kitengo cha usafishaji na udhibiti wa taka  Manispaa ya Morogoro, Samwel Subi, amesema changamoto ya mabadiliko tabianchi ni suala la kidunia kwa ujumla hivyo kikao chao na Balaozi wa Mazingira itampa fursa ya kuona mbinu za Kukabiliana na changamoto hiyo kimkakati.

Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa kitengo cha Maliasili na  Hifadhi ya Mazingira Manispaa ya Morogoro, Dauson Jeremia, amesema Manispaa kwa kushirikiana na wadau wamejipanga kuhakikisha maliasili zinalindwa pamoja na kuongeza kasi ya upandaji wa miti na kusimamia wanaoharibu misitu.

Dauson,amempongeza, Chage, kwa kazi kubwa anaoyifanya kwa kushirikiana na wadau wa mazingira kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.