Header Ads

BONANZA LA WAALIMU SEKONDARI MANISPAA YA MOROGORO LAFAANA


WAALIMU  wa shule za sekondari Manispaa ya Morogoro wamefanya Bonanza la michezo mbalimbali kwa lengo la kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao ,  kuburudika kwa pamoja na kupata mbinu zitakazo saidia wanafunzi wao kufanya vizuri wanaposhiriki michezo mbalimbali.

Bonanza hilo limefanyika Agosti 05/2023 kwenye Uwanja wa Mpira wa Miguu Jamhuri na kutanguliwa na mbio fupi kutoka kwa Vikundi mbalimbali vya Jogging.

Akifungua Bonanza  hilo, Afisa Elimu sekondari wa Manispaa ya Morogoro, Gabriel Paul,  amewapongeza Walimu kwa ushiriki wao na kuwasisitiza kuwa michezo ni afya hivyo watumie nafasi hiyo vizuri kuburudika kwa kucheza michezo mbalimbali.


Kwa upande wa Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Bi. Germana Mung'aho, kipekee amewashukuru wadhamini wa Bonanza hilo CWT, Selous Marathon na wadau kwa kuwezesha Bonanza hilo kufanyika ambapo Walimu wamepata fursa ya kukutana  na kufurahi pamoja.

"Natambua tunafanya kazi kubwa ya kufundisha lakini no vizuri kupata muda wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza" Amesema Bi.Mung'aho.


Naye Katibu wa Chama Cha Waalimu Mkoa wa Morogoro (CWT),Ndg. Alphonce Mbassa, amesema  CWT kinatambua sana umuhimu wa michezo ambapo kwa nyakati tofauti walimu wamepata nafasi ya kushiriki michezo ndani na nje ya nchi.

"Sisi kama CWT Mkoa tukiwa ni walezi wa waalimu, tumeona tuweke nguvu kubwa kudhamini Bonanza hili tukiwa na lengo la kuimarisha mahusiano ya Waalimu na CWT ,rai yangu kuona Mabonanza haya yanakuwa na muendelezo,niombe  Wilaya nyengine ziige mfano wa  Manispaa ya Morogoro" Amesema Mbassa.

Mbassa,amesema CWT itaendelea kudhamini michezo kwa wanafunzi na walimu wa shule za msingi na sekondari huku akiwaomba  wadau wengine kusaidia  kudhamini katika sekta ya michezo ambayo imeanza kuleta manufaa makubwa kwa wana michezo na Taifa.

 Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Johnerick Fredirick, amesema kuwa kupitia mabonanza hayo walimu watakutana,kufahamiana na kuwa na hali  ya kushiriki katika michezo ambayo itaongeza hisia ya mafanikio na uzalendo katika majukumu yao ya kila siku.

Mwenyekiti wa Bonanza hilo,Elias Mosi,amesema  michezo hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa mbinu mbalimbali walimu katika kufundisha michezo wanafunzi ili kuwasaidia kufanya vizuri mashindano ya  shule za  msingi (Umitashumta) na Sekondari(Umisseta).

Katika michezo hiyo, washindi wote waliweza kupata zawadi ya fedha taslimu ambazo waliahidiwa na waandalizi wa Bonanza hilo.

Miongoni mwa waalimu wa Sekondari walioshiriki katika Bonanza hilo, Mwl. Willy Sanga, amewapongeza wadhamini  wa bonanza hilo kwa kuamua kuanzisha mabonanza ya michezo ambayo yatasaidia kuibua vipaji vingi na kuimarisha afya za walimu.

Michezo iliyofanyika katika Bonanza hilo ni  mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa wavu, mchezo wa kuvuta Kamba, kukimbiza kuku na kukimbia ndani ya magunia. pamoja na mchezo wa kuweka ndimu mdomoni kwa kutumia kijiko wenye matembezi ya Mita 100.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.