Header Ads

WACHEPUSHA MAJI MTO RUVU KUMWAGILIA BANGI



OPERESHENI iliyofanyika hivi karibuni katika wilaya tatu za Mkoa wa Morogoro imebaini uwepo wa wakulima wa bangi waliochepusha maji ya Mto Ruvu kwa ajili ya kumwagilia zao hilo.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Agosti 2, 2023 imesema operesheni hiyo iliyoendeshwa siku nane kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama iliwezesha kuteketezwa kwa ekari 489 za bangi, magunia 131 ya dawa hizo za kulevya na kilo 120 za mbegu za zao hilo.

Pia, operesheni hiyo imewezesha kukamatwa kwa watu 18 wanaotuhumiwa kuhusika na mashamba hayo ambayo yapo katika maeneo ya kificho wilaya za Morogoro, Morogoro Vijijini na Mvomero.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema wakulima hao wamejiingiza katika vitendo vya uharibifu wa mazingira ili watimize azma yao ya kulima zao hilo haramu.

“Wakulima wa bangi wa mkoa huu wanachepusha maji na kuyazuia kwenda kwenye maeneo mengine ili kumwagilia mashamba yao,” Amesema Lyimo.

“Wameweka mashamba huku mafichoni wakiamini hawawezi kufikiwa, ila DCEA tumewafikia na tumewakamata. Wamefanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti katikati ya msitu ili waweze kulima bangi, wanachofanya ni kuzidi kuharibu vyanzo vya maji katika maeneo haya na kusababisha changamoto hata kwa maeneo mengine yanayotegemea maji yatoke huku,” Amesema Lyimo.

Lyimo ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaolima bangi na mirungi ili wachukuliwe hatua za kisheria.


CHANZO: MWANANCHI

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.