Serikali yaagiza kuajiri maafisa utamaduni.
SERIKALI imeagiza Mikoa na Halmashauri nchini kuajiri maafisa utamaduni na Maafisa michezo wa muda katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri ili kusaidia kutekeleza majukumu ya kada hizo na kukuza sekta ya utamaduni, Sanaa na michezo katika maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa Agosti 16/2023 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Pindi Chana (Mb) wakati akifungua kikao kazi kilichohusisha viongozi wa Wizara hiyo na wakuu wa Taasisi za sanaa na Utamaduni hapa nchini kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Magadu katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Waziri Dkt. Pindi Chana amebainisha kuwa kati ya halmashauri zaidi ya 180 zilizopo hapa nchini zipo ambazo hazina Maafisa utamaduni na michezo hivyo ameitaka Mikoa na Halmashauri ambazo hazina Maafisa hao kutoa ajira ya muda kwa watumishi wa kada hizo kutokana na umuhimu wa michezo na utamaduni ili kuongeza kasi ya utendaji kazi katika maeneo yao.
“...nimeshatoa maagizo, tuone namna gani katika kipindi hiki cha mpito tunaposubiri vibari vya kuwaajiri rasmi, lazima tuwe na watu wanao kaimu nafasi hizo ili shughuli ziende...lazima Halmashauri, lazima Mikoa iweke mtu anaye kaimu ili kazi ziende...” amesema Dkt. Pindi Chana.
Aidha, Waziri huyo amesema kila Mkoa na Wilaya kuna kamati za michezo ambazo wenyeviti wake ni Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya ambao wanafanya nao kazi ili kuhakikisha kuwa maelekezo yanayotolewa yanafanyiwa kazi kuanzaia ngazi ya chini.
Pamoja na Maagizo hayo Waziri Pindi Chana amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo kwa wananchi katika sekta ya afya, maji, umeme hata kwenye sekta ya michezo ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya michezo pamoja na kujenga mahusiano mazuri ya kiutamaduni na mataifa mengine.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma (Mb) amezitaka taasisi zinazohusika na masuala ya michezo, utamaduni na sanaa kufanya kazi kwa ushirikiano,na kuwataka washiriki kupitia kikao hicho kuweka maazimio ya pamoja ili kuendelea kukuza sekta ya Utamaduni, sanaa na michezo hapa nchini.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akitoa salamu za Mkoa ameipongeza Wizara hiyo kwa kuandaa kikao hicho ambacho kina manufaa katika kukuza sekta ya utamaduni na michezo pamoja na pongezi hizo ameiomba Wizara hiyo kuongeza jitihada zaidi kutoa elimu kwa watanzania kujitambua, kuthamini na kujivunia utamaduni wao.
Kikao kazi hicho kimelenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Wizara hiyo ya Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na wakuu wa Taasisi zinazofanya kazi sambamba na Wizara hiyo zikiwemo Baraza la Taifa la Sanaa, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania na nyingine zilizoalikwa kwenye kikao hicho.
Tweet@chombo huru media,Youtube@chombo huru media, Facebook@chombo huru media, Instagram @chombohuru_media
Post a Comment