DC KILAKALA AAGIZA HALMASHAURI MORO DC NA MANISPAA YA MOROGORO KUTENGA MAENEO YA UWEKEZAJI
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, ameagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Manispaa ya Morogoro kutenga maeneo ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji ikiwamo,maeneo ya kilimo na viwanda vitakavyowezesha kuwepo vitega uchumi vingi katika Wilaya ya Morogoro.
Kauli hiyo ameitoa Februari 10/2025 katika Kikao cha kawaida cha Baraza la Biashara Wilaya ya Morogoro kilichofanyika katika Ukumbi wa Savoy Manispaa ya Morogoro.
DC Kilakala, amesema , maeneo yoyote duniani hayawezi kupiga hatua kimaendeleo na kiuchumi bila viongozi kukaa pamoja kuweka mazingira ya uwekezaji ,hivyo ni muhimu mazingira yatengwe ili yaweze kusaidia kuinua uchumi wa Wilaya ya Morogoro pamoja na kipato cha mtu mmoja mmoja.
"Ili tufanye vizuri katika eneo hili la uwekezaji, tunatakiwa kuandaa kikosi kazi cha Baraza la biashara ambacho lengo ni kutengeneza mikakati ya kutangaza fursa za uwekezaji katika Wilaya yetu"Amesema DC Kilakala.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Morogoro Muadhini Mnyanza,amesema lengo la kikao hicho ni kujadili changamoto za mazingira ya biashara katika Wilaya na kuzipatia ufumbuzi.
"Baraza hili ni jukwa rasmi linalotoa fursa ya majadiliano kati ya Sekta binafsi na sekta za Umma, tunamshukuru Mwenyekiti wetu DC Kilakala,ametupa muelekeo naamini kama yale ambayo tumeyawasilisha yakitekelezwa tutakuwa mbali na wafanya biashara wetu watakuwa kwenye mazingira rafiki na tutaongeza wawekezaji na kuongeza pato la Wilaya pamoja na pato la mtu mmoja mmoja" Amesema Mnyanza.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Manispaa ya Morogoro,John Kilunge, amesema tayari Manispaa imeshatenga maeneo ambayo yatatumika kama vitega uchumi vya Manispaa.
Kilunge ,amesema kuanzia mwanzoni mwa mwezi Machi 2025,watayatangaza maeneo yote ya Vitega uchumi kupitia mabango ya barabarani pamoja na mitandao ya Kijamii na kuwa na Mkutano Mkubwa wa kutangaza maeneo ya vivutio vya utalii na maeneo ya uwekezaji.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimba Madini Mkoa wa Morogoro, Omary Mzeru,amesema kama maeneo ya uwekezaji yakitangazwa pamoja na kuitangaza Sekta ya madini kwa kutengewa masoko ya uhakika Mkoa wa Morogoro utakuwa Mkoa tajiri sana nchini.
Mzee Mzeru,amesema Morogoro ni mkoa wa pili kwa upatikanaji wa Madini nchini lakini bado wanakosa masoko ya uhakika jambo linalrudisha nyuma soko la madini.
Mzeru,ameiomba Serikali kuangalia kwa jicho la tatu Soko la Madini Mkoa wa Morogoro ili wachimba madini waweze kunufaika zaidi na madini wanayochimba na kuongeza pato la Mkoa wa Morogoro.
Post a Comment