Header Ads

WAZIRI PINDA ASEMA MAONESHO YA NANENANE NI TASWIRA CHANYA KWA WAKULIMA


 

WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda,amesema maadhimisho ya  wakulima Nane Nane ni darasa huru kwa wakulima, wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla kwani zinatoa nafasi kwao kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo kilimo chenye tija, Ufugaji wa kisasa na Uvuvi wenye tija pasina kuharibu rasilimali za Serikali.

Hayo ameyasema katika Ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki Katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere  Manispaa ya Morogoro Agosti 01/2023.

Mhe. Pinda, amesema Serikali inatambua kadhia inayowakabili Wakulima nchini hivyo amesema maonesho hayo yatawasaidia wakulima kupata elimu ya pembejeo halisi ikiwamo mbegu, dawa (viuatilifu), mbolea kutoka kwa mashirika husika yanayozalisha pembejeo mbali mbali, ili kuwasaidia kuepuka kununua pembejeo feki ambazo huwasababishia hasara na kuwakatisha tamaa.

"Maonesho haya huwa yanaambatana na Maonyesho ya bidhaa za kilimo yanayofanywa na Wakulima na Mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya kilimo, lengo likiwa ni kutangaza shughuli zao, kubadilishana uzoefu na wataalam wa kilimo kutoka maeneo mbalimbali " Amesema Mhe. Pinda.

Pia, amesema kupitia Maadhisho haya Wakulima wadogo ambao ni wengi ukilinganisha na wakulima wakubwa watajifunza mbinu mpya za kitaalamu za kilimo zinazoendana na wakati uliopo ili kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na ya tabianchi na hatimae walime kilimo cha kisasa kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji.

Hata hivyo,amesema  kwa muda mrefu Wakulima wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea ambacho hakizingatii kanuni za kitaalam, jambo lililowasababisha kukata tamaa na kuona kuwa kilimo hakilipi kutokana na mbinu duni ambazo wamekuwa wakizitumia.

Amesema kuwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi inajipambanua zaidi ili kuwa kwamua Wakulima nchini waondokane na kilimo cha kubahatisha cha kutegemea mvua na badala yake wajikite katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika, kinachoweza kuyabadilisha maisha yao kiuchumi kutokana na mazao mengi watakayopata.

"Natambua kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanategemea Sekta ya Kilimo kama ajira yao sehemu kubwa ya kilimo ni cha Wakulima wadogo wadogo ambao mashamba yao yana ukubwa wa hekta 0.9 na hekta 3.0 kwa kila moja, Karibu asilimia 70 ya ardhi ya kilimo na mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 hutumia maksai na asilimia 10 hutumia trekta hivyo kama  Serikali tutajitahidi kadri iwezekanavyo kuwakwamua Wananchi ili kuondokana na uduni katika mavuno" Ameongeza Mh. Pinda.

Ameongeza kuwa katika maonesho hayo anatarajia Wakulima watajifunza mbinu bora na za kisasa za kilimo zitakazowawezesha kupata mazao mengi na kuinua kipato chao.

Aidha ametoa wito kwa Wakulima na Mashirika kujitokeza katika Maonesho hayo kwa sababu watapata fursa ya kujifunza mambo mengi na kubadilishana uzoefu na wataalam mbalimbali wa kilimo.

Katika Maonesho hayo, Mhe. Pinda,ameambatana na Wakuu wa Mikoa wa Kanda ya Mashariki wakiongozwa na mwenyekiti wa maonesho hayo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Aboubakari Kunenge, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro mwenyeji Mhe. Adamu Malima, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba , Viongozi wa CCM MKoa na Wilaya,  Wakuu wa Wilaya , Wenyeviti wa Halmashuri na Meya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na wakuu wa Taasisi za  UMMA na Binafsi .

Maonesho ya nanenane yameanza Agosti 1 yatamalizika Agosti 8,2023  ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2023 " VIJANA NA WANAWAKE NI  MSINGI IMARA WA MIFUMO ENDELEVU YA CHAKULA".

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.