Header Ads

DC KILAKALA AWATAKA WATAALAM WA AFYA KUHAMASISHA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI JUU YA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE.


MKUU  wa wilaya ya Morogoro ,Mhe.Mussa Kilakala, amewataka wataalam wa afya kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari ili kujikinga na magonjwa yasiyo pewa kipaumbele, ikiwemo ugonjwa wa kichocho, magonjwa ya minyoo ya tumbo hasa kwa watoto chini ya umri wa miaka 15, Trakoma, Matende na Mabusha pamoja na Usubi.

Hayo ameyazungumza Januari 20-2025  katika  kikao cha "PHC" kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa  kikiwa na lengo la kupanga mpango mkakati wa zoezi la umezeshaji dawa za kichocho na minyoo ya tumbo shuleni. 


DC Kilakala,  amewataka wataalam wa afya, kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uwepo wa choo kwa kila kaya, kwani kwa kufanya hivyo, kutapunguza kuenea kwa magonjwa.

Vilevile, DC Kilakala,  amewaomba wataalam hao kuwahamasisha wananchi kuwa na utaratibu ya kupima afya mara kwa mara ili kupunguza athari zitokanazo na magonjwa yasiopewa kipaumbele.

Aidha, DC Kilakala,  ametoa shukrani kwa Mhe. Rais na serikali ya awamu ya sita, Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa namna inavyojali wananchi hata kufanya haya mazoezi ya chanjo na umezaji dawa, ili kulinda jamii na watoto dhidi ya magonjwa mbalimbali yasiyopewa kipaumbele.


Aidha amewaomba viongozi wa dini kutumia nafasi zao katika kuisaidia serikali kufikisha Elimu kwa waumini wao ili kupata jamii ambayo itafahamu kwa ukaribu magonjwa haya yasiyopewa kipaumbele na kuchukulia tahadhari.


Naye Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga,  amesema kwa kuzingatia njia zote za kujikinga au kupiga vita magonjwa haya hususani magonjwa ya kichocho na minyoo ya tumbo, Manispaa  inaweza ikatokomeza magonjwa haya na kusiwe na maambukizi yoyote.

Kwa upande wa  Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Mkoa wa Morogoro, Debora Kabudi C,amesema Serikali imetumia gharama kubwa kuhakikisha inatokomeza magonjwa haya ili wananchi wake waishi vizuri, na kutengeneza kizazi chenye afya nzuri ya mwili na akili.

Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele Manispaa ya Morogoro,  Warialanga Nnko amesema Manispaa imekuwa na muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa Taifa wa kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.


NNko,amesema, Manispaa inatarajia kuendesha zoezi la umezeshaji dawa kuanzia Januari 27-28 mwaka 2025.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.