MAITI ZAKUTWA KANDO YA BARABARA KENYA
WAKAZI wa Birongo, eneo bunge la Nyaribari Chahe, wamelalamikia hali mbaya ya usalama katika eneo hilo.
Tukio la hivi karibuni la usalama ambalo limetokea tarehe 3
Agosti 2023, limeacha wakazi wakiwa na hofu baada ya wanaume wawili kupatikana
wametupwa kando ya barabara.
Akithibitisha tukio
hilo la kusikitisha, OCPD wa Kisii Central, Amos Ambasa, amesema mkono na miguu
ya mmoja wa wanaume hao vilikuwa vimefungwa na walikuwa na majeraha kichwani.
Ambasa amesema alipokea ripoti kutoka kwa mkuu wa eneo hilo
kwamba walikuta miili ya wanaume wawili wenye umri kati ya miaka 25 na 40.
Kutokana na uchunguzi wao wa awali, inaonekana wawili hao
walikuwa wameuawa sehemu nyingine kabla miili yao kutupwa eneo hilo, ambalo ni
mpaka kati ya kaunti za Nyamira na Kisii.
''Leo asubuhi tulipokea ripoti kutoka kwa mkuu wa eneo la
Birongo kwamba kuna miili ya wanaume wawili vijana, wenye umri wa miaka 25, na
mmoja mwenye umri wa miaka 40. Hatujui bado kilichotokea, lakini tangu tufike
eneo la tukio, tumegundua kwamba miili yao ina majeraha yanayofanana.
Inaonekana vitu vyenye ncha kali na vitu vingine vikubwa vilitumika", amesema Ambasa.
Mkuu wa polisi amesema kazi yao imekuwa rahisi baada ya
kuwafahamu jamaa wa wanaume hao wawili, na ameongeza kwamba watasaidia
kufuatilia harakati zao kabla ya mauaji.
Post a Comment