MWALIMU AUAWA KINYAMA, MTOTO WAKE AJERUHIWA
Mwalimu wa
Shule ya Msingi Nyakatundu iliyopo Rufiji mkoani Pwani, Rafaela Msemwa ameuawa
kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Agosti 6, 2023.
Pamoja na
kutekeleza unyama huo, watu hao pia walimjeruhi mtoto wake mwenye umri wa miaka
minne, aliyejulikana kwa jina la Bravian Mwamwenda na kumsababishia jeraha
kubwa usoni na kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Mpaka sasa
Bravian ameendelea kupokea matibabu kutoka kwa wataalamu bingwa na tayari
wamemfanyia upasuaji wa jicho na wanasubiri kumfanyia vipimo vingine kuangalia
iwapo jicho hilo litaweza kuona tena.
Hayo
yamesemwa na baba mdogo wa marehemu, Nolasko Msemwa akiwa nyumbani kwao
wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe kuhusiana na mauaji hayo.
Mwili wa
Rafaela umesafirishwa kutoka Rufiji kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya
taratibu nyingine za maziko.
Akizungumzia
suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Rufiji, Protas Mutayoba amekiri
kutokea kwa tukio hilo na amesema tayari uchunguzi umeanza ili kuwabaini
waliohusika na mauaji hayo.
“Tukio
limetokea usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili Agosti 6, huyu mama ni mwalimu wa
Shule ya Nyakatundu, aliuawa na watu ambao hawajulikani na wakamuumiza mtoto wake
mdogo wa miaka minne, kwa hiyo tunaendelea kufuatilia kuona namna ya kuwapata
hawa waliotenda kosa hilo,” amesema kamanda huyo.
Kwa mujibu
wa RPC, Mwalimu Rafaela alikuwa anaishi peke yake na mtoto wake kwenye nyumba
ya shule na ni mgeni eneo hilo ametokea Tarime, mkoani Mara.
“Kwa mujibu
wa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Rufiji, tangu amehamia shuleni hapo hajafikisha
miezi mitatu,” amesema Kamanda Mutayoba.
Akizungumzia
namna walivyobaini mauaji hayo, Kamanda Mutayoba amesema ni baada ya mwalimu
mwenzake kufika nyumbani hapo akimfuata waende kanisani kama ilivyokuwa miadi
yao ya siku ya Jumamosi jioni.
“Kuna
mwalimu ambaye ni jirani yake, ndiye aliyegundua mauaji hayo. Jioni waliagana
kwamba atampitia waende wote kanisani, ilipofika asubuhi akawa anamtafuta ili
waende, sasa akawa hapatikani kwenye simu, ikabidi aende nyumbani kwake ndiyo
akakutana na hali ile,” amesema kamanda huyo.
Amesema kwa
upande wa Jeshi la Polisi tayari wameanza msako; “kazi yetu ni lazima
tufanikishe kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliotenda uovu
huu, kama ni mmoja au wengi tupo kazini, tunafanya upelelezi wetu na tutawatia
mbaroni tu’’.
Kwa upande
wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Michael Gwimile
amesema Rafaela alikuwa mtumishi wa halmashauri divisheni ya elimu ya awali na
msingi.
“Halmashauri
na menejimenti imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo chake na inatoa pole kwa
ndugu, jamaa na marafiki,” amesema Gwimile.
Msiba wa
mwalimu huyo uko nyumbani kwa shemeji yake maeneo ya Ubungo Makoka, jijini Dar
es Salaam.
Post a Comment