MWANAMKE MBARONI, ADAIWA KUMILIKI SMG KIENYEJI
POLISI mkoani Rukwa, inamshikilia Shangwe Lodrick (35),
mkazi wa Mtaa wa Bangwe, Kata ya Izia, Tarafa ya Lwiche, Manispaa ya
Sumbawanga, akidaiwa kumiliki bunduki aina ya Shotgun, iliyotengezwa kienyeji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija, amesema
hayo leo Agosti 3, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake, ambapo pia ametoa taarifa ya kukamatwa kwa pikipiki nne zilizoibwa na
kutumika kwenye matukio ya uhalifu.
Kamanda Masija amesema bunduki hiyo iliyotengenezwa kienyeji
ilikamatwa ikiwa pamoja na risasi 8 zinazotumika kwenye vitendo vya uhalifu.
"Wasamaria wema watupa taarifa ambapo polisi walifika
nyumbani kwa mwanamke huyo na kufanya upekuzi na kukuta silaha hiyo ambayo inadaiwa
imekuwa ikitumika kupora fedha kwenye visima vya mafuta na maduka yanayotoa
huduma za kifedha kwa mitandao ya simu," amesema.
Amesema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya
upelelezi kukamilika ili sheria ziweze kuchukua mkondo wake.
Katika hatua nyingine, polisi imefanikiwa kukamata pikipiki
sita ambazo ziliibwa maeneo tofauti tofauti mkoani hapa, pikipiki mbili kati ya
hizo zimetambuliwa, huku watuhumiwa wakitarajiwa kufikishwa mahakamani.
Kamanda huyo amewataka wananchi walioibiwa pikipiki kufika
kituo kikuu cha polisi Sumbawanga ili waweze kuzitambua pikipiki zao.
CHANZO: MWANANCHI ePaper
Post a Comment