Header Ads

WAKUU WA SHULE , WENYEVITI WA BODI NA MAAFISA ELIMU KATA WATAKIWA KUINUA UFAULU SHULENI

 

WAKUU  wa Shule za Sekondari ,Wenyeviti wa Bodi pamoja na Maafisa Elimu Kata Manispaa ya Morogoro  wametakiwa kusimamia elimu ili kufikia malengo ikiwa ni pamoja na kukuza ufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza, la pili na la tatu lakini pia kupunguza kiwango cha wanafunzi wanaofeli.

Wito huo umetolewa na Meya Manispaa ya Morogoro Mhe. Khalid Matengo ,  wakati akizungumza katika kikao kazi cha Tathmini ya matokeo ya Kitaifa ya mwaka 2025 kwa Shule za Sekondari katika Ukumbi wa Bwalo Shule ya Sekondari Kilakala.

Meya Matengo , amesema   malengo ya Halmashauri katika upimaji wa kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2025 ni kufuta daraja sifuri na kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anayemaliza kidato cha nne anapata cheti lakini pia kupunguza ufaulu wa daraja la nne na kuongeza ufaulu bora yaani daraja I, II, na III.

Aidha,amesisitiza suala la upatikanaji wa chakula Shuleni huku akiwataka Wazazi kutoa ushirikiano katika hilo.

Pia, amewataka wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wakiwa shule na nyumbani ili kuongeza ufaulu .

Hata hivyo,amewataka walimu kuwa wabunifu Zaidi kwa kutumia mbinu mbadala za kufundisha ili wanafunzi waende na kazi ya walimu.

Mwisho,amezitaka shule zenye maeneo makubwa kujikita Zaidi katika kilimo cha mboga ili kupata lishe bora kwa wanafunzi.

Akiwasilisha taarifa ya matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2025, Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari, Sylevester  Mwenekitete, amesema kuwa  matokeo sio mabaya kwa  kwa  wanafunzi wa kidato cha pili waliopimwa na kidato cha nne  hivyo ameomba jitihada za makusudi ziongezwe ili Manispaa katika matokeo ya mwaka 2026 iwe ya Kwanza Kimkoa na Kitaifa.

Katika hatua nyingine, Mwenekitete, amewapongeza wakuu wa shule ambao shule zao zimefanya vizuri na kuwataka kuziendeleza jitihada hizo huku akiwataka wakuu wa shule ambazo hazikufanya vizuri kuongeza jitihada ili wapate matokeo mazuri katika mitihani inayofuata.

Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za Uchumi, Afya na Elimu Manispaa ya Morogoro, Mhe. Spear Komanya, amesema ili ufaulu uongezeke lazima nidhamu kwa walimu na wanafunzi iimarishwe pamoja na kuwajengea uwezo walimu kujifunza kwa wenzao waliofaulisha Zaidi.

Naye  Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Euphrasia Buchuma, amewataka wakuu wa shule pamoja na Maafisa Elimu Kata kusimamia nidhamu shuleni ikiwa ni pamoja na kuzuia utoro wa wanafunzi pamoja na walimu ili kuinua taaluma kwani vitendo hivyo huathiri tendo la ufundishaji na ujifunzaji.

 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.