PROF. KABUDI AIPONGEZA SERIKALI KUJA NA TEKNOLOJIA YA KISASA YA UGAVI WA VIFAA VYA KUJIPIMA NA KUZUIA MAAMBUKIZI MAPYA YA VIRUSI VYA UKIMWI NA KUIASA JAMII KUCHUKUA TAHADHARI.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi amepongeza Teknolojia ya kisasa ya ugavi wa vifaa vya kujipima na kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Hayo ameyasema katika ziara ya kikazi Mkoani Morogoro Julai 03 alipotembelea Kituo cha Afya Kingolwira Manispaa ya Morogoro, Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) na Chuo Kikuu Mzumbe.
Prof. Kabudi ,amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia miradi mbalimbali inayosimamiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS katika udhibiti wa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
"Hii ni Teknolojia ya kisasa ambapo Tanzania ni miongoni mwa Nchi duniani tunaotumia teknolojia hii, tumenunua kwa mapato yetu ya ndani ni mashine za kisasa za hali ya juu duniani, wito wangu ni kuendelea kuamasihana juu ya matumizi ya mashine hizi na kuendelea kuvitunza vifaa hivi kwani vimenunuliwa kwa gharama kubwa ikiwa ni nia njema ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI" Amesema Prof. Kabudi
Aidha, Prof. Kabudi , ameiasa jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini ili kuunga mkono jitihada za Serikali dhidi ya mapambano hayo na kuyafikia malengo yaliyopo.
Amesema malengo ya Serikali katika kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi ni utoaji wa elimu ya kutosha kwa jamii , kuongeza idadi kubwa ya mashine za kujipimia za kisasa, kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Pia,amesema kufuatia kwa wahisani kupunguza usaidizi kwa Serikali, mikakati mikubwa ya Serikali ni kuhakikisha Vifaa tiba vinatengenezwa hapa nchini ikiwemo kujenga Viwanda vya uzalishaji wa dawa za ARV hata kwa zaidi ya asilimia 60 ifikapo mwaka 20230 pamoja na kutengeneza chanjo za watoto na chanjo nyengine.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Mussa Kilakala, amesema jamii haina budi kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine kwa kuzingatia ushauri na elimu inayotolewa ili kuhakikisha hali ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini ipungua na kuyafikia malengo ya kuzifikia sifuri tatu ifikapo 2030.
Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Adam Mrisho, amesema kuwa, Tume iendelee kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Kondomu ili kupunguza maambukizi ya VVU na UKIMWI hasa kwa kundi la vijana nchini hususani kwenye mikusanyiko kama vile vyuoni kwa kuweka mashine za kisasa za teknolojia za kujipima.
Dkt. Adam amesema kwa sasa Tanzania ina jumla ya mashine 10 ambazo imezifunga kwenye vyuoni vikuu 4 na mpango uliopo ni kuongeza mashine 65 ili kuendelea kuhamasisha wananchi kujua namna bora ya kujilinda na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI.
“TACAIDS imeendelea kufanya kazi nzuri ya kuifikia jamii kwa njia ya elimu, ila endeleeni kuongeza nguvu kwa vijana kwani ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi bila kusahau ni kundi muhimu katika uzalishaji na kujiletea maendeleo yetu, hivyo elimisheni kwa nguvu watu wabadili mitazamo yao,”Amesema Dkt. Mrisho.
Naye Mratibu wa huduma za UKIMWI, Magonjwa ya ngono na homa ya ini Mkoa wa Morogoro , Dkt. Shigela Marco, amesema Mkoa wa Morogoro una jumla ya vituo 584 vya kutolea huduma za afya, vituo 151 vinatoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU ,vituo 446 vinatoa huduma kinga za VVU na matibabu ya magonjwa ya ngono ,vituo 474 vinapima VVU, vituo 1192 ni maeneo ya upimaji wa VVU ndani ya vituo na vituo 383 vinatoa huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito na kujifungua wakati wa unyonyeshaji .
Dkt. Shigela ,amesema , Januari hadi Machi 2026 jumla ya wananchi 122, 026 walijitokeza kupima VVU , wananchi 1,348 sawa na asilimia 99 walikuwa na VVU ya lengo kwa robo (1,348/1,365) na waliweza kupewa rufaa kwenda vituo vinavyotoa huduma ya tiba na matunzo na kuanzishiwa dawa za ARV.










Post a Comment