JUMUIYA YA AHMADIYYA MOROGORO YATOA MSAADA WA VYAKULA KWA ZAIDI YA KAYA 200 ZENYE UHITAJI.
Hafla hiyo fupi ya ugawaji wa vyakula imefanyika Machi 15 /2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ahmadya Kihonda Maghorofani.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la ugawaji wa vyakula,Meya Manispaa ya Morogoro akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Khalid Matengo, ambaye ndiye mgeni katika hafla hiyo, ameushukuru Uongozi wa Ahmadyya, kwa kujitoa kwao hususani katika kutoa huduma ya elimu kwa kuwa na shule zao, huduma ya afya katika Hospitali zao pamoja na kutoa huduma ya kiroho.
"Wenzetu Ahmadyya licha ya kugawa zawadi hii katika kuwajali ndugu zetu kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, lakini wanatukumbusha kuwa na upendo pamoja na kusaidiana, hili sio jambo dogo , ni jambo la kiimani lenye kumpendeza Mwenyezi Mungu, ukiwa na roho ya uchamungu hata mambo yako yanafanikiwa"Amesema Matengo.
Meya Matengo , amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanawalea katika maadili ya kumcha Mungu ili kuweza kuwa na Viongozi watakaoongoza Tanzania katika imani na misingi ya Kimungu.
Aidha, Meya Matengo , amewataka Wazazi kujitoa katika kujifunza jinsi ya kuwalea watoto katika misingi halisi ya kumjua Mungu.
Kwa upande wa Amiri na Mabshiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Tahir Mahmood Chaudhry, amesema kuwa dini ya kiislamu ni dini ya amani na upendo na dini yenye mafundisho ya kujaaliana kama wanajamii.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Kihonda Maghorofani, Eng. Mhe. Hamisi Ndwata, ameupongeza Uongozi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Ahmadiyya Morogoro kwa kuwajali wananchi na kuweza kula pamoja Sikukuu hiyo.
Mhe. Ndwata, amesema Jumuiya hiyo mbali na kugawa vyakula kwa wenye mahitaji , lakini imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia mambo mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa wamekuwa wakijitoa saana.
"Mimi binafsi naridhika sana na ushirikiano wa Jumuiya hii, wamekuwa karibu sana na Jamii lakini hata katika kushiriki mambo ya maendeleo wamekuwa mstari wa mbele sana kuchangia, hivyo nawaomba mwakani panapo uzima wagawe vyakula kwa idadi kubwa ya watu zaidi ya hapa" Amesema Ndwata.
Naye Mkuu wa Chuo cha Jumuiya ya Ahmadiyya Morogoro, Sheikh Abid Mahmood Bhatti, amesema kuwa msaada huo umetolewa kuunga mkono wito wa serikali inayohimiza mashirika,taasisi,na watu binafsi kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji.
Bhatti, amesema licha ya kuunga mkono Serikali lakini pia kuweza kutoa zakatul Fitri kwa jamii ili kuweza kujumuika na jamii katika kusherehekea Sikuu ya Eid Fitr.
"Jumuiya ya Ahmadiyya ni moja ya sehemu inayojihusisha na utoaji wa misaada mbalimbali ikiwemo ya kiafya,kielimu na kijamii kwa kuwafikia watu wenye uhitaji, hivyo kutoa kwetu chakula kwa watu wenye uhitaji kwanza tumetekeleza misingi ya dini , kwani sisi tumekuwa tukifanya hivi kila ifikapo Siku ya Eid basi tumekuwa tukijumuika na ndugu zetu kuhakikisha kwamba tunakuwa nao pamoja katika kusheherekea sikukuu hii " Amesema Bhatti.
Bhatti, ameeleza msimamo wa jumuiya ya Ahamdiyya kwamba ni jumuiya inayohubiri amani na upenda kwa wote bila chuki kwa yeyote na inahubiri huheshimu dini zote na kuishi katika mazingira ya kuhurimiana .
Miongoni wa vyakula hivyo vilivyo gharimi takribani zaidi ya Shilingi milioni 4 na zaidi, ni pamoja na Mchele mfuko wenye Kilo 5 na Unga wa Sembe Mfuko wa Kilo 10.





















Post a Comment