Header Ads

HUMANITY FIRST TANZANIA KWA KUSHIRIKIANA NA AHMADIYYA MUSLIM JAMAAT TANZANIA YATOA NGUVU KAZI KUSAFISHA SHULE YA MSINGI JUHUDI LUKOBE

SHIRIKA  la Humanity First Tanzania (Utu kwanza) kwa kushirikiana na Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania, imetoa nguvu kazi ya vijana wake kushiriki katika usafishaji wa Shule ya Msingi Juhudi iliyopo Kata ya Lukobe kufuatia shule hiyo kuathirika na mvua kubwa zilizopelekea madarasa ya shule kuingia matope pamoja na miundombinu mengine ya shule kuathirika.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa usafi huo, Mratibu wa Shirika la Humanity First Tanzania Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya utoaji wa misaada mbalimbali katika Majanga , Shekh Abid Mahmood, amesema wametoa msaada huo  wa kusafisha Shule kama moja ya kazi zao zinazofanywa na Shirika hilo pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na miundombinu iliyo athirika na mafuriko.

"Tumefika hapa kwa kuguswa kwetu na majanga ya mafuriko, sisi kama Shirika la utu kwanza, kazi yetu ni kusaidia jamii na hiki tulichokifanya ni moja ya jukumu letu lakini kuiunga mkono Serikali ambayo imekuwa ikipambana sana na maeneo ambayo yameathirika na mafuriko" Amesema Sheikh Mahmood.

Naye Afisa Elimu Kata ya Lukobe, Leonard Mtete kwa niaba ya Diwani wa Kata na Baraza la Maendeleo la Kata, ameishukuru Shirika la Humanity First Tanzania (Utu kwanza) kwa kushirikiana na Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania kwa kujitoa kwao kwani usafi huo utawaruhusu moja kwa moja wanafunzi Jumatatu kuhudhuria shuleni  kwani shule imekuwa safi tofauti na awali ambapo vyumba vya madarasa viligubikwa na matope mazito.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Juhudi , Naomba Msuya, ameshukuru ushirikiano wa Shirika na Ahmadyya kwani madarasa yalikuwa na hali mbayo na sasa watoto wanaweza kuyatumia.

Katika usafi huo, Maafisa Afya Manispaa ya Morogoro waliendesha zoezi la ugawaji wa dawa ya Chlorione kwa wananchi kwa ajili ya kuzuia vijidudu vya virusi na bakteria kwenye maji. 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.