MANISPAA YA MOROGORO YAADHIMISHA WIKI YA UNYONYESHAJI WA MAZIWA YA MAMA DUNIANI
MANISPAA ya Morogoro imeadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Dunani yanye lengo la kutoa hamasa kwa jamii katika kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa watoto.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro,Mhe.Mussa Kilakala,Agosti 07-2025 katika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Akizungumza juu ya maadhimisho hayo, DC Kilakala, amewataka wakina mama wote ambao wamejifungua watoto na wanaotarajia kujifungua kutoa kipaumbele katika suala la unyonyeshaji wa ziwa la mama kwani faida zake huchangia katika uchumi wa nchi.
Aidha, DC Kilakala,ametoa wito kwa watoa huduma wa afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuendelea kuhakikisha wanafikia jamii na elimu ya unyonyeshaji wa ziwa la mama ,lishe na afya kwa ujumla inatolewa ipasavyo.
DC Kilakala,amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kutambua umuhimu katika kuhudumia jamii na kuhakikisha katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji anawajengea uwezo zaidi kuhusiana na ulishaji wa watoto wachanga na wadogo ambapo unyonyeshaji wa ziwa la mama ni mada muhimu ndani yake.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Manispaa ya Morogoro, Dkt.Maneno Focus, amewataka watoa huduma wahakikishe maeneo waliyopo wanawawezesha jamii kutambua umuhimu wa ziwa la mama na kuhakikisha ufanishaji wa ziwa la mama unazingatiwa.
Mratibu wa Kitengo cha Lishe Manispaa ya Morogoro, Ester Kavishe,amesema mtoto akizaliwa ndani ya lisaa limoja annyonyeshwe apate maziwa ya awali ya majimaji ya njano yanayoitwa kolostaramu ambayo ni bora sana kwa mtoto ambao katika kipindi cha miezi sita anyonyeshwe ziwa la mama pekee bila kupewa chakula chochote.
Kavishe,amesema maziwa ya mama ni chakula bora kwa mtoto kwani humpa mtoto virutubisho vyote kwa uwiano sahihi na pia maji katika miezi sita ya mwanzo.
Mwakilishi wa wazazi,Anna Mwakipesile,amesema tangia ajifungue amekuwa akizingatia mlo kamili na unyonyeshaji sahihi kitu kilichofanya watoto wake kuwa na afya njema kutokana na kuzingatia makundi sita ya chakula.
Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani, yamebeba Kauli Mbiu ya wiki ya unyonyeshaji mwaka 2025 "Thamini Unyonyeshaji: Weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto" ambapo Maadhimisho hayo yyalianza tarehe 1 - 7 Agosti, 2025 kupitia vituo vyote vya kutolea huduma za Afya.
Post a Comment