Header Ads

MKUU WA WILAYA MOROGORO, AWATAKA WASIMAMIZI WA VITUO VYA UCHAGUZI KUZINGATIA SHERIA , KANUNI , TARATIBU NA MIONGOZO KUFANIKISHA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA KWA AMANI.



MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amewataka wasimamizi wa Vituo vya Uchaguzi kuhakikisha wanasimamia vyema Sheria, kanuni , taratibu pamoja na miongozo ili uchaguzi uwe wa haki na amani bila ya uvunjifu wowote wa amani.
Hayo ameyasema leo Novemba 23, 2019 , wakati wa ufunguzi wa Semina ya mafunzo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi iliyoandaliwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba.
Amesema kuwa anatambua kwamba maandalizi ya uchaguzi yamepita katika hatua mbali mbali muhimu ambapo kuanzia Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kutoa Tangazo la uchaguzi Tarehe 28, Septemba 2019.
Aidha, amewakumbusha kwamba bado wasimamizi wa Uchaguzi wana wajibu wa kupitia kanuni za Uchaguzi ya mwaka 2019 pamoja na Mwongozo hususani katika maeneo ya taratibu za upigaji kura (kanuni ya 32-34) upigaji kura (Kanuni ya 35-37) kuhesabu kura na kutangaza matokeo (kanuni ya 38-39) pamoja na mwongozo wa Uchaguzi (ukurasa 13-17).
"  Niwaombe Wasimamizi wa Vituo vya Uchasguzi, maeneo hayo niliyoyataja mkiyasoma kwa umakini mtaweza kufanya na kukamilisha Uchaguzi wetu kwa amani na utulivu, mkatende haki na muhakikishe Walemavu, Wazee, Wagonjwa, Mama Wajawazito pamoja na wanaonyonyesha muwape vipaumbele kwani hili ni kundi muhimu sana lililopewa nafasi yake katika jamii" Amesema DC Chonjo.
Mwisho  ni matarajio yangu kuwa mtaifanya kazi hii mliyopewa kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, huku akiwatakia kila la kheri katika uchaguzi huo.
Amesema kuwa, hatua zote alizozitaja kama zitafanyika kwa waledi mkubwa na kwa kuzingatia miongozo ni matumaini yake makubwa kwamba zoezi la upigaji wa kura litakwenda vizuri na kwa waledi wa hali ya juu bila ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa Wananchi na wagombea kwa ujumla.
Aidha ameongeza kuwa  Serikali kwa kutambua umuhimu wa Uchaguzi huo, imejipanga vizuri na vifaa vyote muhimu  kwajili ya Uchaguzi vimeshaletwa na kupokelewa, hivyo amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa maandalizi mazuri ya Uchaguzi.
"Niwaombe Wasimamizi wa Vituo pamoja na Wasimamizi wasaidizi wa Kata na Mitaa , mnawajibu wa kuhakikisha vifaa vya Uchaguzi vinatunzwa ili baadae vije kutumika kwa Chaguzi nyingine zijazo, unatakiwa kuwa mwaminifu , mchapakazi, muadilifu, mzalendo na mzingatiaji maadili na Utumishi wa Umma" Ameongeza kusema DC Chonjo.
Kwa upande wa Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Ndg. Waziri Kombo, amesema Wasimamizi wa Vituo wana wajibu wa kupanga, kusimamia na kuendesha uchaguzi katika misingi inayowezesha Uchaguzi kuwa huru na haki na kwa kufuata Katiba ya Nchi, Kanuni za Uchaguzi na Sheria nyingine za Nchi.
"Washiriki wa mafunzo haya naomba niwakumbushe mmepewa dhima kubwa sana ya kusimamia jambo ambalo lina maslahi mapana kwa ustawi wa Nchi yetu katika nyanja zote za kiuchumi, kisisasa, kijamii, kiutamaduni na Kidemokrasia fanyeni kazi vizuri tuzidi kulinda amani ya Taifa letu"" Amesema Waziri Kombo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuweza kufika na kufungua mafunzo hayo, lakini kubwa zaidi amewataka Wasimamizi wazingatie muda wa kufungua vituo kwa kufuata kanuni na Mwongozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 na kama walivyoelekezwa katika mafunzo.
Pia amewataka Wasimamizi wasasidizi wa Vituo wahakikishe wanasimamia zoezi la Uchaguzi katika vituo vyao bila kujali jinsia, kabila , Chama na hali yoyote aliyonayo mpiga kura kwa mfano watu wenye ulemavu wa aina yoyote.
Msimamizi Msaidizi kituo cha Geza Ulole Kata ya Kauzeni , Mtendaji wa Mtaa wa Kauzeni, Ahmad Juma Almas, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa kuanzisha mafunzo hayo kwani yamewakumbusha wajibu wa kufanya kazi na kujenga uaminifu na kujizua na vitendo vya rushwa.
Naye Dorica Uledi,ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Uluguru, amesema semina hiyo imewasidia kwa upande wa kujua wajibu wao hivyo ameahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha zoezi la uchaguzi linakamilka kwa amani.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.