Header Ads

MIAKA MINNE YA JPM , MADIWANI MANISPAA MORO WAMPONGEZA KWA KUIPATIA FEDHA NYINGI ZA MIRADI YA MAENDELEO UKIWEMO WA UJENZI WA SOKO KUU JIPYA LA KISASA.

Posted On: November 2nd, 2019
BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk John Magufuli, kwa kutoa fedha Sh bilioni 17.6 zilizowezesha kujengwa soko jipya la kisasa lenye ghorofa moja ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 76.
Soko hilo linajengwa baada ya Wizara ya fedha kupitia Hazina kuipatia halmashauri hiyo , kiasi cha fedha hizo baada ya soko la zamani iliyojengwa mwaka 1953 kuwa chakavu na kuvunjwa .
Meya wa Manispaa hiyo , Pascal Kihanga alitoa shukurani hizo wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Oktoba 31, 2019 mjini hapa akiunga mkono hoja mbalimbali za madiwani walipokuwa wakichangia ajenda za kikao hicho.
Kihanga alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kuipatia fedha nyingi katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk Magufuli.
Katika ujenzi wa soko hilo alisema , ujenzi utarajiwa ukamilike Septemba 19 mwaka huu ( 2019) lakini kutokana na sababu mbalimbali , mkandarasi Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi ya Nandhra iliomba kuongezewa muda na kupewa hadi Februari 2020 , ujenzi uwe umakamilika.
“ Baraza hili haina budi kumpongeza Rais kwa kutupatia fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa kituo cha afya cha Mji Mpya , barabara za lami pamoja na fedha zaidi ya bilioni 17 za kujenga soko kuu jipya ambalo ujenzi wake hadi sasa umefikia asilimia 76” alisema Kihanga
Alisema , kwa niaba ya wananchi wa Manispaa hiyo anaeendelea kumshukuru Rais na kusema, ujenzi wa soko hilo ni miongoni mwa miradi endelevu itakayoiingizia halmashauri mapato yatakayosaidia kuboresha huduma za kijamii.
“ Kwa muda mfupi wa uongozi wake tumepata fedha nyingi za maendeleo , ujenzi wa soko kuu jipya , pia kuwezesha stendi ya mabasi ya Msamvu kurudi mikonini mwa Manispaa , haya ni mafanikio makubwa na tunampongeza na kumwombea maisha marefu” alibainisha Kihanga.
Hata hivyo aliwatoa hofu wafanyabiashara kuwa, wataendelea kutekeleza makubaliano waliokubaliana awali kwa wafanyabiashara waliokuwa soko la zamani kabla ya kuvunjwa kupisha ujenzi huo watakuwa wa kwanza kupewa vizimba vya kufanyia biashara zao.
“ Ujenzi wa soko hili utakapokamilika kipaumbele kitawekwa kwa wafanyabiashara waliopisha ujenzi wapo zaidi ya 1,000 ambao tumewapeleka kwa muda soko la Manzese na litaluwa na eneo la wafanyabiashara wa mboga na litakuwa na vibanda vingi vya maduka zaidi ya 160 na maeneo ya kutolea huduma mbalimbali za kijamii” alisema Kihanga.
Naye Diwani wa Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Doroth Mwamsiku alisema , Serikali ya awamu ya tano imewezesha mambo mengi ya maendeleo nchini na kwa Manispaa ya Morogoro imenufaika na kupatiwa fedha hizo za kujenga soko kuu jipya ambalo litachagia upatikanaji wa mapato yakutosha kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.