Header Ads

MKURUGENZI MANISPAA MOROGORO AFUNGUA MAFUNZO YA UZINGATIAJI WA KANUNI, SHERIA NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA KWA MAKATIBU MAHSUSI, WAHUDUMU, MAKARANI MASJALA, WALINZI PAMOJA NA MADEREVA





MKURUGENZI wa Manipsaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, leo Novemba 11, 2019, amefungua  mafunzo ya uzingatiaji wa kanuni, sheria na taratibu za Utumishi wa Umma kwa Makatibu Mahsusi, Wahudumu, Makarani masjala, Walinzi pamoja na Madereva kwenye ukumbi wa Kilimo Manispaa Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari , amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo juu ya uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Amesema kuwa mafunzo hayo yameendeshwa na wawezeshaji kutoka Chuo kikuu Mzumbe , hivyo amewaomba watumishi kuzingatia mafunzo hayo  muhimu kwani yanawajengea uwezo watumishi kimaadili katika kazi  za kila siku.
"Tumewaandalia mafunzo haya ikiwa ni sehemu ya wajibu wangu kama mwajiri wenu wa kuwajengea uwezo ili hatimaye muweze kuongeza ufanisi wa kazi kila mmoja katika eneo lake la kazi, nyinyi ni watu muhimu sana kwenye taasisi yoyote, nawaomba mjiamini vya kutosha ,muwe familia moja na ukipigiwa simu pokea maana muda mwingi tunautumia ofisini,  mungu amekupa ulinzi wake , cheo kikiondoka tayari nuru inaondoka , tujiepushe na majungu ila ukiwa na wazo la kuboresha , ofisi yangu ipo wazi karibuni kwa ajili ya kuijenga Manispaa yetu" Amesema  Sheilla.
Aidha, amekipongeza Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kujitoa kwao katika ushirikiano wa mafunzo hayo pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, akisema matarajio yake ni kwamba baada ya mafunzo hayo watumishi wataacha kufanya kazi kwa mazoea na wataenda kuwatumikia wananchi kwa kutoa huduma bora pamoja na kutunza siri za ofisi.
Mbali na mafunzo hayo, amewataka watumishi kujiunga na vikoba kwani mishahara waliyoanyo haiwatoshi katika kuendeleza familia zao.
Amesema vikoba vinasaidia sana , kwani wataongeza vipato na kuweza kuendesha familia kama vile kusomesha watoto pamoja na kuwa na biashara ndogo ndogo zitakazo wawezesha kujikwamua kimaisha.
Naye Afisa Utumishi wa Manispaa ya Morogoro Waziri Kombo, amesema mafunzo hayo yamehudhuriwa na jumla ya watumishi 99, huku akitarajia kila mtumishi mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo watumishi wataachana na utendaji kazi wa mazoea.
Amesema  kuwa, wamewalenga hao kwanza kwani wao ndio wasaidizi katika ofisi pamoja na kutunza siri za ofisi, hivyo amewataka wabadilike na kuendana na kasi ya Mhe.Rais Dkt John Magufuli ya kuchapa kazi kwa bidii pamoja na kufuata misingi ya utawala bora.
" Niwaombe watumishi wenzangu, tusifanye kazi kwa mazoea, wengi wetu tunafanya kazi kwa mazoea, sheria , ukiangalia kanuni na sheria pamoja na kimtazamo wa ufanyaji kazi umebadilika, Rais wetu anahitaji matokeo chanya kwa maendeleo ya Taifa,  hivyo lazima tubadilike ili kuendana na kasi yake na asiye badilika tutamchukulia hatua za kisheria " Ameongeza Kombo
Aidha amesema baada ya mafunzo hayo, watakuja kufanya mafunzo kwa wakuu wa idara mbali mbali wa Manispaa ya Morogoro ili nao kuwajengea uwezo wa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa Umma.
Katika hatua nyengine,  Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni msaidizi kumbu kumbu, Bi: Anastazia Mgimba, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa  kuandaa mafunzo hayo kwani yatawajengea uwezo mkubwa wa kuwatumikia wananchi na kutoa huduma bora ikiwamo kutunza siri za ofisi pamoja na kuzingatia sheria na kanuni  na taratibu za Utumishi wa Umma.
Kwa upande wa William Paul Mollen, ambaye ni Askari wa Jeshi la akiba Manispaa ya Morogoro, amesema wao wameyapokea mafunzo hayo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wakufunzi wa mafunzo kwani yataleta tija kubwa katika utoaji wa huduma bora.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.