Header Ads

JUMLA YA KATA 9 NA MITAA 27 KUSHIRIKI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA NOVEMBA 24,2019.

Posted On: November 22nd, 2019
MSIMAMIZI  wa Uchaguzi  Serikali za Mitaa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Ndg. Waziri Kombo, ametangaza Kata na Mitaa inayotarajiwa kushiriki  katika zoezi la  Uchaguzi Serikali za Mitaa siku ya Jumapili Novemba 24,2019.
Ratiba hiyo ameitoa leo mapema Ofisini kwake, ambapo zoezi hilo litahusisha jumla ya Kata 9 na Mitaa 67 ambazo zitashiriki katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Kwa nafasi ya wenyeviti wa mitaa ,wajumbe kundi mchanganyiko,na wajumbe kundi la wanawake.
Amesema kupungua kwa Vyama vya Siasa katika kushiriki   zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Manispaa ya Morogoro kumetokana na Vyama vya Upinzani kujiondoa katika kushiriki Uchaguzi na kusababisha baadhi ya maeneo  wagombea wa Chama Tawala CCM kupita bila kupingwa.
Aidha, amezitaja Kata zitakazoshiriki zoezi la Uchaguzi Serikali za Mitaa, Miongoni mwa Kata hizo ni pamoja na Kata ya Uwanja wa Taifa ,Mafisa,Tungi,Luhungo,Mindu,Chamwino,Mkundi,Mazimbu, na Kauzeni.
 Amesema katika Mitaa yote kwenye kata zinazoshiriki Uchaguzi Serikali za Mitaa , vipo vyama vya siasa vilivyoshiriki katika maombi ya kujaza fomu lakini baadhi ya  wagombea wao walijiondoa na hiyo kupelekea wagombea wa CCM katika Kata hizo na Mitaa kupita bila kupingwa.
"Jumapili Novemba 24, 2019 utafanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo kwa nafasi yangu ya Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Morogoro nimeona nitoe taarifa juu ya uchaguzi huu ,lakini kama unavyoona katika taarifa  ni kwamba wapo wagombea wa Vyama vya Upinzani walishiriki zoezi la kujaza  fomu za uchaguzi, lakini wapo wagombea ambao walikosa sifa kwa mujibu wa sheria zilizopo na wengine waliopita katika maombi walijiengua  kufuatia matamko ya  kauli za Viongozi wao wa juu" Amesema Waziri Kombo.
Amevitaja vyama vilivyoshiriki katika kuchukua fomu za Uchaguzi Serikali za Mitaa kabla ya Wagombea wao hawajaenguliwa na wengine kujitoa, miongonii mwa vyama hivyo ni  Chama cha Mapinduzi CCM, United Democratic Party (UDP) pamoja na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mbali na hayo, amewaasa na kutoa rai kwa  Wananchi kutofanya fujo katika uchaguzi na kuwataka wale wote waliojiandaa kufanya fujo kuacha mara moja kwani watakao bainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.