Header Ads

KAMATI YA FEDHA, UONGOZI NA MIPANGO MANISPAA YA MOROGORO YAFANYA ZIARA YA KUTEMBELEA MIRADI YA UJENZI WA SOKO KUU LA KISASA PAMOJA NA MRADI WA UJENZI WA STENDI MPYA YA DALA DALA LEO NOVEMBA 14/2019.




Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga (wapili kutoka kulia), kati kati Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mhe Isihaka Sengo, pamoja na Mwenyekiti wa Mipango Miji, (kushoto), Mhe Diwani  wa Kata ya Mwembe Songo, Ally Rashid Kalungwana wakipata maelekezo mafupi mara baada ya kutembelea mradi wa Soko Kuu la Kisasa Morogoro.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba (kulia), Mstahiki Meya wa Manispaa Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga (wapili kutoka kulia, Naibu Meya Manispaa Morogoro , Mhe. Isihaka Sengo (watatu kutoka kulia) pamoja na Mwernyekiti wa Mipango Miji , Mhe Diwani Ally Kalungwana wakipeana maelekezo wakati wa ziara ya Kamati ya Fedha na Mipango kutembelea Mradi wa Soko Kuu la Kisasa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Mradi wa Ujenzi wa Soko Kuu la Kisasa Halmashauri ya Manispaa ya  Morogoro ukiendelea na kasi ya ujenzi na maendeleo ulipofikia hadi sasa kwa asilimia 75%.

Mradi wa Ujenzi wa Soko Kuu la Kisasa Halmashauri ya Manispaa ya  Morogoro ukiendelea na kasi ya ujenzi na maendeleo ulipofikia hadi sasa kwa asilimia 75%.

Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa, Mhe. Pascal Kihanga, Naobu Meya wa Manispaa, Mhe. Isihaka Sengo , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Morogoro, Sheilla Lukuba, Mhandisi wa miradi ya benki kuu ya dunia pamoja na mahandisi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Eng. Juma Gwisu wakishauriana jambo wakati wa zaiara hiyo.
KAMATI ya Fedha, Uongozi na Mipango Halmashauri  ya  Manispaa yav Morogoro leo Novemba 14, 2019, imefanya ziara ya kutembelea miradi mikuu miwili inayotekelezwa ndani ya manispaa hiyo, ikiwamo mradi wa  Kimkakati wa Ujenzi wa Soko kuu la kisasa Kata ya Mji Mkuu, pamoja na mradi wa Ujenzi wa Stendi mpya ya Daladala iliyopo Kata ya Mafiga.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa  Halmashauri ya Manispaa ya  Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema lengo la kutembelea miradi hiyo ni  pamoja na kuangalia maendeleo ya miradi hiyo ilipoishia na inavyoendelea.

Aidha, Mstahiki Meya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema katika ziara hizo mbili walibaini kutokuwepo na kasi nzuri ya ufanyaji wa kazi japo maendeleo yeke yanaridhisha, hivyo ametoa agizo kwa wakandarasi wote wawili wanaosimamia miradi hiyo wafanye kazi usiku na mchana ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwahudumia wananchi.

Katika upande wa mradi wa Kimkakati ulipatiwa ruzuku na Serikali ,katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mhe Kihanga, amemtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kwa ajili ya kuwawezesha Wananchi  kupata huduma  bora za kiuchumi na kijamii.

Amesema matarajio yake katika mradi huo ni kwamba hadi kufikia Desemba 31 , mwaka huu 2019 , mradi huo utakuwa umekamilika.

Amesema mradi huo pindi utakapokamilika utawahudumia zaidi ya wafanyabiashara 1500, huku kipaumbele cha kupewa maeneo ya biashara kitatolewa kwa Wafanyabiashara waliokuwa wanafanya biashara awali kabla ya soko la zamani kuvunjwa.

" Mhandisi tunakwama wapi? unajua wakati Naibu Waziri wa fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alipofanya ziara hapa tulikuwa katika kasi kubwa sana, nashangaa sasa hivi kasi ya ujenzi imepungua, sasa hebu tushirikiane Mkandarasi, Mshauri wa mradi pamoja na Manispaa tuwe kitu kimoja , tunapo kwama tuambiane na kama kuna shida ya fedha ziombeni kwani pesa zipo zinatusubiria sisi na ikifika desemba 31 hizi fedha zitaondoka na tutazikosa , sitaki tuzikose maana zikiondoka nyinyi wakandarasi mtakosa fedha na sisi tutakosa fedha na tutakuwa tumekwamisha huu mradi unaotegemeawa kutoa huduma kubwa na kuingizia pato taifa pamoja na Manispaa yetu" Amesema Mhe. Kihanga.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema wataendelea na ziara za kutembelea miradi hiyo mara kwa mara kwani miradi hiyo imetengwa kwa lengo la kuifanya mamlaka za Serikali za Mitaa za  Manispaa ya Morogoro ziweze kujitegemea kimapato.

Amesema mradi huo utagharimu Shilingi Bilioni 17,ambapo pindi mradi huo utakapokamilika Halmashauri inategemea kukusanya takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 2.7 kwa mwaka hivyo itapunguza kutegemea ruzuku toka Serikali kuu.

Licha ya kuridhishwa na  hatua za mradi huo iliyofikiwa katika utekelezaji  , lakini aliwataka wale wote wanaosimamia mradi huo kuzidisha kasi ya ujenzi, na kuona mkanadarasi anakuwa site masaa ishirini na nne kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kuzuia upotevu wa fedha za Wanyonge zinazotekeleza mradi huo.

Upande wa Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Eng. Juma Gwisu, amesema ujenzi huo mpaka sasa umefikia asilimia 75%, na wanatarajia kukamilisha mwishoni mwa mwaka huu Desemba 31, mwaka 2019.

Mwenyekititi wa Mipango Miji , Ally Rashidi Kalungwana , amesema wao kama Kamati ya fedha, uongozi na mipango , hawatachoka kufanya ziara hizo kwani kufanya ziara hizo kunasaidia miradi mingi kwenda  kwa kasi.

Naye Kelvin Chacha, msimamizi wa maradi, amesema kuchelewa na kusua sua kwa mradi huo kumetokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi ambazo ni kuwepo kwa mtandao wa maji taka (MORUWASA), uwepo wa wingi wa maji eneo la mradi (High table) uvunjaji wa misingi wa majengo ya soko la zamani, pamoja na mvua zilizonyesha kipindi cha hivi karibuni.

Katika hatua nyengine, Mhandisi wa Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Nadra Engineering Construction Company Ltd, Eng. Charles Richard, amesema ujezni huo utakuwa na Maduka 304, Meza 900, maeneo makubwa 16 ya kupangishwa kwa mita za mraba (benki, maduka makubwa , ofisi nk) maegesho ya magari makubwa 5 ya mizigo kwa pamoja, maegesho ya magari madogo 143 kwa pamoja, vyoo, migahawa, stoo 36 za mitumba, bucha pamoja na eneo la kuchinjia kuku.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.