MKURUGENZI MANISPAA MOROGORO AAHIDI USHIRIKIANO NA WAMACHINGA ,BAADA YA KUKABIDHIWA CHETI NA SHIRIKA LA WAMACHINGA TANZANIA.
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheila Edward Lukuba, ameahidi kuendeleza Ushirikiano dhidi ya Wafanya biashara ndogo ndogo maarufu Wamachinga kufuatia Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) kwa upande wa Manispaa ya Morogoro , kuikabidihi Manispaa hiyo Cheti kutokana na ukaribu na ushirikiano mkubwa wa kuwawezesha Wamachinga kujiendeleza.
Akizungumza leo Novemba 5, 2019, Ofisini kwake, katika kumwakilisha upokeaji wa cheti hicho kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa John K.Mgalula, Mkurugenzi Sheila, amesema anatambua umuhimu wa Wamachinga , hivyo Manispaa yake itaendelea kushiriki na kuwa karibu na Wafanya biashara hao.
Amesema ni vyema Wamachinga wakathaminiwa, kwani hata Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, amekuwa mstari wa mbele katika mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara na kuwatambua kama kundi muhimu kuelekea Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa kati.
"Nashukuru sana kwa mchango wenu, kwanza mmetupa heshima Manispaa, mnatambua umuhimu wa Serikali yenu nasi tutazidisha mahusiano bora na rafiki kwenu ili kuhakikisha wafanya biashara wote mnanufaika na mnakuwa na kipato katika biashara zenu, haiwezekani wachache wanufaike wengine muumie, tutawasimamia kama Mh Rais wetu Dkt John Magufuli anavyo wathamini, nakipokea cheti hiki kumwakilisha Mkurugenzi aliyepita , natumani taarifa zenu anazo, tusichoke kwenye changamoto tuambiane sisi kazi yetu ni kuwakwamua pale mnapo kwama" Amesema Sheila.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Sheila, amesema kundi hilo linatambulika kwa kupatiwa Vitambulisho vya Wajasiriamali kwa malipo ya Shilingi Elfu 20,000/=tu kwa mwaka, hivyo wawe makini na wafanya biashara wanaojifanya wao ni Wamachinga kwa lengo la kukwepa kodi ya Serikali.
"Sisi Manispaa tunahitaji kodi, kuna watu wajanja wajanja sana wanajifanya wamachinga kumbe wanakwepa kodi, tukiwashtukia tutawashughurikia, tunahitaji kodi kwa ajili ya maendeleo, tuna miradi ya Hospitali, Shule, Maji, Maabara na mengineyo yote inahitaji fedha" Amesisitiza Sheila.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Shirika la Umoja Wamachinga Tanzania ( SHIUMA) , Ndugu Faustine France, amesema Cheti hicho ni kwa heshima ya Manispaaa pamoja na Mkurugenzi aliyepita kwa kuwatambua na kuwathamini.
"Naipongeza Manispaa kwa kazi nzuri za ujenzi wa Taifa pamoja na usimamizi mzuri wa miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ya Kimkakati , Jumuiya yetu tunaahidi kwa dhati kukupatia ushirikano kama ilivyo kwa Mkurugenzi aliyepita katika Manispaa yako, tupo tayari kufuata maelekezo yako na tutayafanyia kazi" Amesema Faustine.
Aidha, amesema licha ya kutoa cheti hicho, pia ugeni wao ulikuwa ni pamoja na kumkaribisha Mkurugenzi mpya kwa kumpa ushirikiano na kutambua wamachinga pamoja na Jumuiya yao kwa Maendeleo ya Manispaa ya Morogoro.
Post a Comment