Header Ads

"Walimu jengeni utaratibu wa kuwafundisha Wanafunzi kujua thamani ya pesa inayotumika katika Miradi ya Shule" : MURUGENZI Manispaa Morogoro.




Mkurugenzi wa Manispaa Morogoro , Sheilla Lukuba, (kati kati), kushoto Afisa Elimu Msingi Manispaa Morogoro, Ndug. Abdul Buhety wakielekezwa jambo na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msamvu "B".
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewaasa Walimu wa Shule za Msingi pamoja na Sekondari kujenga tabia ya kuwafundisha wanafunzi wao juu ya thamani ya pesa inayotumika katika miradi ya shule.

Tamko hilo amelitoa jana akiwa katika ukaguzi wa Mitihani ya Darasa la nne, hii ni kutokana na  uharibifu wa Majengo ya Shule uliofanywa na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mji Mpya  hivi karibuni wakati wa wanafunzi wa kidato cha nne wakimaliza mitihani yao ya Taifa.

Amesema Serikali imetumia fedha nyingi katika Miradi hiyo kwa kuwekeza katika elimu hususani mpango wa elimu bure bila malipo ulioasisiwa Chini ya  Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.

Aidha, amewataka Wanafunzi kuwa Watoto wema pamoja na kuwasikiliza Wazazi na Jamii inayowazunguka ikiwamo kulinda na kutunza rasilimali za Shule kwa maendeleo ya Vizazi vijavyo.

"Waalimu niwaombe, kaeni na Wanafunzi wenu muwaambie thamani ya pesa iliyotumika katika uwekezaji wa Majengo shuleni, kwani pesa hizi zimetokana na kodi za Watanzania Wanyonge, na Serikali ni wananchi hivyo majengo haya yakianza kutumika vibaya kwa kuharibiwa unafikiri waliotoa pesa zao watatufikiriaje? je tukiomba tena tutapewa? mjitathmini kama kuna Mwanafunzi mnamuona hawafai toeni taarifa achukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria kuliko kuwalea na kuleta madhara kama haya kwa Serikali, kuweni na huruma Serikali inajitahidi kuhakikisha Wanafunzi wanaishi katika mazingira rafiki ili wasome vizuri" Amesema Sheilla.

Aidha amewaasa Wanafunzi wenye tabia ya kuharibu mazingira pamoja na majengo ya Shule huku akisema Serikali ina mikono mirefu kwani watakapo gundua kuna mwanafunzi amefanya vitendo hivyo atakuwa amejiharibia maisha yeke na ndoto zake.

Pia ametoa wito kwa Waalimu wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogroro, kusimamia miundombinu ya shule kikamilifu hususani katika miradi inayotekelezwa na Serikali Shuleni kwani kufanya hivyo kutasaidia kuendelea kutoa elimu bora kwa vizazi vijavyo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.