Header Ads

Mkuu wa Wilaya Morogoro, amtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kufanya tathmini ya kupitia upya sheria katika kutatua changamoto ya kodi inayowakabili Wafanyabiashara wa Vibanda vya SUA Road Kata ya Masika.





MKUU wa Wilaya Manispaa ya Morogoro, Mhe Regina Chonjo, amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, kufanya tathmini upya juu ya sheria za biashara katika kuweka mazingira rafiki na Wafanya biashara wa Vibanda vya SUA Road vilivyopo Kata ya Masika.

Agizo hilo amelitoa leo Novemba 7, 2019 kwenye Viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, kufuatia malalamiko ya Wafanya biashara hao ya kuongezewa kodi kutoka Shilingi 30,000/= hadi Shilingi 50,000/=.
Akizungumza na Wananchi hao katika kulitolea majibu suala hilo, DC Chonjo, amemtaka Mkurugenzi kukaa chini pamoja na watendaji wake wapitie upya sheria na kuona jinsi gani wanaweza kufikia muafaka wa kupunguza kodi hiyo wanayolipa kwa sasa ili wafanya biashara hao waweze kufanya biashara zao na kujipatia kipato.

Amesema Mkurugenzi afike pale  na kuzungumza na Wafanya biashara hao wakubaliane , kwani kitendo cha wafanya biashara hao kufunga vibanda hivyo kinawakoseshea mapato Manispaa pamoja na wafanya biashara hao wanakosa ridhiki katika kujikimu na maisha.

"Nikuombe Mkurugenzi, fuatilia jambo hili kwa ukaribu sana, kaeni pamoja muone jinsi gani mnaweza kufikia muafaka, hawa ni wananchi wetu, na wao wanatafuta ridhiki, wakifunga kwa sababu ya kuongezewa kodi sio jambo jema kwani hata sisi Manispaa tunakosa mapato ni bora tukubaliane kwa kuwapunguzia kodi lakini na sisi pia tupate mapato" Amesema DC Chonjo.

Aidha, DC Chonjo, amesema mahala popote kwenye biashara , huwa kunafanyika tathmini, tathmini hiyo ni pamoja na kuangalia maeneo ya biashara,mtaji wa mfanya biashara katika eneo husika , aiana ya biashara pamoja na tozo husika itakayopangwa kulipwa na mafanya biashara.

Akijibu kuhusu kero ya kutokuwepo kwa Choo katika Vibanda hivyo, DC Chonjo, ametoa agizo kwa Manispaa kuhakikisha wanatengeneza Choo na kukodisha kwani wapo Vijana wengi wanahitaji lakini wakishindwa watafute mdhabuni wa kutengeneza choo ili Manispaa wafanye kazi ya kukusanya kodi.

"Wewe humlishi Ng'ombe unataka ukamue maziwa, haiwezekani kaeni mtengeneze hicho choo, kwani huwezi kukusanya kodi ukashindwa kuwawekea huduma muhimu kama hiyo" Ameeleza DC Chonjo.
Naye upande wa mwakilishi wa Wafanya biashara wa Vibanda vya Tope Road, Jackson Busanda, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa maamuzi yake huku akisema watashukuru sana kama Manispaa itawapunguzia kodi hiyo.

" Nimefurahishwa sana na maambuzi ya Mkuu wa Wilaya, kwa kweli tupo katika hali ngumu, Shilingi 50,000/= ni kubwa sana sasa tumefunga vibanda vyetu hatujui hatima itakuwaje tuna familia endapo Manispaa itatupunguzia kodi tutaendelea na biashara zetu na manispaa watapa mapato kwani hatukatai kulipa kodi ila kodi ni kubwa tunayotozwa kwa sasa" Amesema Jackson


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.