HALMASHAURI YA MANISPAA MOROGORO KUSHIRIKIANA NA ASASI MBALI MBALI ZAJIPANGA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA UKIMWI.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro kwa kushrikiana na Wadau mbali mbali
ikiwamo Asasi waanza maamndalizi ya kuweka
mipango madhubuti ya kupambana na Maambukizi ya Ukimwi.
Hayo ameyasema leo Novemba 28, 2019, kwenye kikao cha mwisho cha maandalizi ya Siku ya Ukimwi Duniani
inayoadhimishwa Desemba mosi kila mwaka.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika kikao cha mwisho cha kuelekea
maadhimisho hayo, mratibu wa Ukimwi wa Manispaa Morogoro , Pendo Elias, amesema maandalizi yanaendelea vizuri hivyo
wapo kwenye mipango mikakati ya kuhakikisha wanapunguza na kuzuia kuongezeka
kwa kasi ya maambukizi mapya ya VVU.
Katika kikao hicho kilichokutanisha wadau mbalimbali ikiwamo asasi za
kupambana na maambukizi ya Ukimwi, Pendo amesema maadhimisho ya mwaka huu mbali
ya kutoa huduma ya kupima virusi vya Ukimwi, kutakuwa na huduma ya upimaji
saratani ya shindo ya kizazi, kisukari na shinikizo la damu.
Pia, Pendo amesema elimu itatolewa kwa makundi tofauti ya watu wakiwamo
vijana ambao ndiyo kundi kubwa linaloonekana kuathirika, watu wanaojihusisha na
biashara ya ngono na wanafunzi hasa wa vyuo kuhusu madhara ya Ukimwi na
unyanyapaa.
Awali, akifungua kikao hicho kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro,
Michael Waluse amesema takwimu za maambukizi ya Ukimwi za manispaa hazipendezi
hivyo lazima kila mdau aweke nguvu ya kupambana na maambukizi mapya badala ya
kuachia kazi hiyo halmashauri.
Waluse amesema lengo la Rais John Magufuli la kuwa na Tanzania ya viwanda
haliwezi kufanikiwa kama wananchi hususan vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa
haitakuwa na afya bora na matumaini ya kuishi.
Maadhimisho hayo yatafanyika Siku ya Jumapili 01, Desemba, 2019 kwenye Maeneo ya Viwanja vya Shule ya Msingi Mwembesongo na kuambatana na Kongamano litakaloanzia Ofisi za Manispaa Saa 2:30 Asubuhi.
Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mhe. Abdulaziz M. Abood, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini.
Ikumbukwe kuwa, Manispaa ya Morogoro Maambukizi ya virusi vya Ukimwi
yamefikia asilimia 4.5 kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa kwenye vituo vya
afya na huduma ya mkoba.
Post a Comment