Header Ads

MSIMAMIZI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA MANISPAA YA MOROGORO ARIDHISHWA NA ZOEZI LA UPIGAJI KURA


Msimamizi wa Uchaguzi Serikali za Mitaa Manispaa ya Morogoro, Ndug. Waziri Kombo.
MSIMAMIZI Uchaguzi Serikali za Mitaa Manispaa ya Morogoro, Ndug. Waziri Kombo,amewapongeza Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo vya kupigia kura baada ya kuridhishwa na hali ya utulivu na mwenendo mzima wa zoezi hilo ulivyokwenda.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema mpaka sasa zoezi linakwenda vizuri na hakuna malalamiko yoyote yaliyojitokeza hivyo inaonesha ni jinsi gani wasimamizi walivyokuwa makini na wanafanya zoezi hilo kwa haki.
Aidha, amesema kuwa vituo vyote vilikuwa na idadi ya kutosha ya wapiga kura waliojitokeza, na wasimamizi wa Uchaguzi walifika mapema kwa kuzingatia muda uliopangwa.
" Nimeridhishwa na hali ya zoezi la upigaji kura hakuna kituo ambacho hakijafunguliwa, vituo vyote vilikuwa wazi, sijapokea malalamiko yoyote hadi sasa, hii inaonesha kwamba zoezi linakwenda vizuri, hivyo matumaini yangu hadi kufunga zoezi hili mambo yatakwenda vizuri, niwapongeze wasimamizi wa vituo vya uchaguzi niwaombe waendelee kutimiza majukumu yao kwa kufuata misingi ya haki ili kila mtu aweze kutimiza haki yake ya msingi ya kikatiba" Amesema Kombo.
Amesema Manispaa ya Morogoro kwa zoezi la upigaji kura ilikuwa na jumla ya kata 29 zenye Mitaa 294, lakini kata zilizoshiriki uchaguzi ni Kata 9 na Mitaa 27, kupungua kwa idadi ya kata na Mitaa kumetokana na  baadhi ya wagombea hususani Chama Cha Mapinduzi kupita bila kupingwa na wagombea wengine wa vyama vya upinzani wakijiengua katika uchaguzi huo.
Ametoa rai kwa Wananchi waendelee kujitokeza kupiga kura kwa muda uliobakia kwani ni haki yao ya kikatiba ya kuwachagua Viongozi watakaoweza kuwaletea maendeleo.
"Niwaombe muende kupiga kura, Uchaguzi huu ni muhimu kwa Ustawi wa nchi yetu, kwa haya masaa mawili yaliyobakia yanatosha kwa wananchi kwenda kupiga kura ,kwani usipopiga kura utajikosesha haki yako ya kikatiba pamoja na maendeleo yako mwenyewe kwakuwa utapata kiongozi ambaye atadumu kwa muda wa miaka 5 hivyo mtaendelea kuteseka kwa kipindi hicho" Ameongeza Waziri Kombo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.