ZIARA YA MKUU WA WILAYA MOROGORO , CHANGAMOTO YA MIGOGORO YA ARDHI YAONGOZA, DC AMWAGIZA AFISA ARDHI KUSHUGHULIKIA KWA HARAKA .
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe Regina Chonjo leo Novemba 7, 2019 amekutana na kusikiliza, kutatua kero za wananchi wa Manispaa ya Morogoro katika viwanja vya hospitali ya Rufaa Morogoro , changamoto nyingi zilijitokeza lakini kubwa zaidi ni Mogogoro ya ardhi kufuatia wananchi kutoa kero zao katika mkutano huo.
Akizungumza na Wananchi katika mkutano huo, DC Chonjo ametoa maagizo mazito kwa Afisa Ardhi mteule wa Manispaa Gisbert Msemwa kuhakikisha migogoro hiyo inapatiwa ufumbuzi pamoja na kutoa taarifa ya utatuzi wa kero hizo ofisini kwake kwa kuonesha jinsi gani migogoro hiyo ilivyo shughulikiwa kwa haki bila vimelea vya rushwa wala uonevu.
“Afisa Ardhi wa Manispaa nakuomba ufanyie kazi na kuzishughulikia hizi kero, haiwezekani kero hizi zinatokea na kurundikana huko mitaani nyie mpo mnaangalia, sasa nataka utekelezaji wa hali ya juu, hawa ni Wananchi wetu, Serikali hii ya awamu ya tano chini ya Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli, inataka kuona migogoro ya ardhi inamalizika na wananchi wanaishi katika hali ya usawa hususani hawa wanyonge ambao wamekuwa wakionewa sana na matajiri aidha kwa kuporwa ardhi yao au mashamba yao" Amesema DC Chonjo.
Katika hatua nyingine, DC Chonjo, amezitaka kero zote za mashamba zilizopo katika Manispaa ya Morogoro, zipelekwe kwa Watendaji wa Kata na kwa kushirikiana na ofisi ya Ardhi na mipangomiji kero hizo zipate majibu.
Amesema kuwa, baada ya kero hizo kuzipokea anataka kupata taarifa zitakazoonesha jinsi walivyoshughulikia kero hizo kwa haki bila ya upendeleo huku akiwaonya watendaji wasiposhughulikia kero hizo atawachukulia hatua za kisheria.
Kwa upande wake Afisa Ardhi Msemwa amesema maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya, kuhusiana na migogoro ya ardhi iliyojitokeza kwa Wananchi, atafatilia na kuifanyia kazi na mara baada ya migogoro hiyo kupatiwa ufumbuzi watakabidhi taarifa hizo kwa Mkuu wa Wilaya.
Hata hivyo Msemwa amesema katika mkutano huo uliofanyika leo, wamepokea kero mbali mbali za migogoro ya ardhi zikiwa katika makundi mbali mbali, ambapo amesema miongoni mwa makundi hayo migogoro ya kimipaka ya viwanja na Mashamba, Ndugu kudhurumiana, pamoja na kundi la watu wanaodhurumiana mashamba.
Naye Mwananchi, Nuru Sultani amepongeza Mkuu wa Wilaya kwa kufanya mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi.
“Kwa kweli mkuu wa wilaya tunaomba ufikishe salamu zetu kwa Mhe.Rais kwa kuchagua viongozi kama nyie wenye maono ya kushughulikia kero za wananchi , tunawombea kwa Mungu awazidishie muendelee kutusikiliza sisi wanyonge” Amesema Nuru.
Post a Comment