Header Ads

ASILIMIA 90 YA WATU WA MKOA WA MOROGORO WAMESAJILIWA NIDA.



MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) mkoa wa Morogoro imeeleza kuwa, hadi sasa asilimia 90 ya wakazi wa mkoa huo wamesajiliwa na kupata namba za vitambulisho ambazo zinawawezesha pia kusajili line za simu zao kwa njia ya alama za vidole.
Ofisa wa Nida wa mkoa huo ,James Malimo alisema hayo alipokuwa akijibu kero juu ya ucheleweshaji upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ambacho pia kwa sasa kinatumika kusajilia line za simu kwa njia ya alama za vidole .
Malimo alisema hayo Novemba 7, 2019 baada ya kutakiwa na mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo kwenye mkutano wake aliouitisha kukutana na wananchi wa wilaya hiyo kila mwezi akianzia na Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi.
Malimo alisema akijibu swali la msingi lililoulizwa na mkazi wa Kola A , Samson Msemembo ambaye alitaka kujua hatua mbalimbali za zoezi la utoaji wa vitambulisho vya Taifa unaoendela kufanyika .
Mkazi huyo alisema , licha ya zoezo hilo kuendelea lakini bado watu wengi hawajaandikishwa na muda wa kufikia ukomo wa kusajili line za simu kwa njia ya alama za vidole wa Desemba 31, mwaka huu unakaribia na watafanyeje iwapo hawatapata kitambulisho hicho baada ya muda huo.
Malimo alisema , Nida ilianza kusajili wananchi kupata kitambulisho cha taifa muda mrefu , lakini baada ya tangazo la Serikali la kusajili upya namba za simu kwa njia ya alama za vidole na kutumia kitambulisho cha taifa , idadi kubwa ya wananchi wanajitokeza ili kutaka kujisajili na kupata kitambulisho cha taifa.
Alisema , baada ya kuona changamoto ya watu kuwa ni wengi na hawajasailiwa , Nida mkoa wa Morogoro iliamua kurudisha mashine za usajili ngazi za kata kuanzia Machi mwaka huu ili kuongea kasi ya uandikishaji na ujazaji wa fomu za Nida.
“ Mpango huu umeleta mafanikio kwani hadi sasa asilimia 90 ya wakazi wa mkoa wa Morogoro wameshasajiliwa na namba za vitambulisho vimezalishwa na zimewasaidia watu kuweza kusajili line zao kwa njia ya alama za vidole kupitia namba ya Nida waliopata “ alisema Malimo.
Hata hivyo alisema ,katika Manispaa ya Morogoro yenye kata 29 ,ni kata moja pekee ya Mji Mpya viongozi wake hawajafika kuchukua orodha ya namba za vitambulisho na kuhimiza kufanya hivyo.
Pia alisema , Nida mkoa wa Morogoro imeongeza muda wa kufanya kazi hadi saa 11 jioni siku za kazi badala ya kutoka saa uliopangwa wa saa 9: 30 alasiri na kwa siku ya jumamosi utoaji wa huduma kwa wananchi itandelea kufanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 7 : 30 mchana.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa mitaa na kata za Manispaa ya Morogoro kuwandaa utaratibu utakaowezesha kuwafikia wazee katika ngazi ya kata ili waweze kuhudumiwa kupatiwa vitambulisho vya taifa .
“ Ninachowaomba watendaji wa mitaa na kata ili kuweza kuwafikia wazee maeneo hayo na makundi mengine watuandalie utaratibu maalumu wa kuwahudumia “ alisema Malimo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.