Header Ads

Semina ya Mafunzo ya uzinduzi wa kupanga mipango na Bajeti ya lishe Mkoa wa Dar es Salaam yazinduliwa rasmi











SEMINA ya mafunzo ya  uzinduzi wa Kupanga Mipango na Bajeti ya Lishe Mkoa wa Dar es Salaam imezinduliwa Leo Kimkoa kwenye Wilaya ya Ilala, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakari Kunenge,  kwenye Ukumbi wa Anautogro Jijini Dar es Salaam .

Akizungumza na Waandishi wa Habari ,  RAS Kunenge  , amesema lengo la Mafunzo hayo ni kuhakikisha mipango ya Lishe inaandaliwa kwa pamoja ili kuleta tija na kutokomeza Utapiamlo na udumavu.

Hivyo amesema ni dhahiri kuwa lishe bora katika jamii ni kichocheo cha maendeleo katika nyanja zote (Afya, Kilimo, Elimu, Biashara, Uchumi, nk).

Amesema kuwa  pale tu ambapo athari za lishe duni au utapiamlo zitakapodhibitiwa au kutokomezwa ndipo malengo ya maendeleo katika nyanja hizi yataweza kufikiwa kwa ufanisi Hivyo amesema Jambo la msingi ambalo watu wanapaswa kulifahamu na kulizingatia ni ukweli kwamba Lishe ni suala mtambuka na utapiamlo katika jamii ni matokeo ya mkusanyiko wa matatizo mengi.

Ambapo  Matatizo hayo yanaweza kusababishwa na ulaji duni na mtindo wa maisha usiofaa, maradhi mbalimbali, kutokuwa na uhakika wa chakula, matunzo duni ya mama na watoto, mazingira machafu, rasilimali haba na mgawanyo usiokuwa na uwiano sahihi kijinsia, umaskini wa kipato, machafuko ya kisiasa na hata sera zisizotambua umuhimu wa lishe kwa maendeleo ya mwanadamu na taifa kwa ujumla wake.


Amesema kuwa Takwimu za Lishe kimkoa za (smart savey ya lishe) kwa mwaka (2015) zilibaini kuwa utapiamlo sugu (UDUMAVU) ni tatizo kubwa ambapo kati ya watoto 712,223 chini ya umri wa miaka mitano, watoto wenye udumavu ni 99,711 sawa na 14.6%, watoto 712,223 wa chini ya miaka mitano, watoto 33,475 wana ukondefu ni sawa na 4.7%.

 Pia amesema Watoto wenye upungufu hii inaonesha kuwa kuwa kuna  kazi kubwa ya kufanya ili kukabiliana na matatizo hayo ya lishe hasa unapoangalia namba halisi ya walioathirika na utapiamlo.

Amewataka wadau wafahamu kwamba lishe bora katika siku 1,000 za mwanzo wa maisha ya mtoto, yaani tangu mimba kutungwa mpaka mtoto anapotimiza miaka miwili, ndiyo msingi thabiti wa ukuaji wa mwili na maendeleo yake ya kiakili.

Amesema kuwa Wataalam wanashauri kuwa watoto waliopata huduma bora na sahihi za lishe, katika kipindi cha siku 1,000 za mwanzo wa uhai wao wanapata faida zitakazodumu katika maisha yao yote ikiwa ni pamoja na maendeleo mazuri ya ukuaji wa ubongo, uwezo mzuri wa kukabiliana na maradhi, uwezo mkubwa wa akili za utambuzi (higher IQ), uwezo mkubwa na ufanisi wa kujifunza na uwezo mkubwa zaidi wa kujiingizia kipato wakiwa watu wazima.

Katika hatua nyingine amesema  bahati mbaya madhara ayapatayo mtoto katika ukuaji wake kimwili na maendeleo ya kiakili kutokana na lishe duni katika siku hizo 1000 za mwanzo za maisha yake hayawezi kurekebishwa tena baada ya kipindi hicho kupita na yataendelea kumuathiri kwa maisha yake yote.

Hata hivyo amesema kuwa  Serikali kwa kutambua kuwa lishe sasa ni suala la kimaendeleo hapa Tanzania, mapambano dhidi ya lishe duni yamekuwa ni mojawapo ya maeneo ya kipaumbele katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); Mpango unaolenga kutekeleza Dira yetu ya Maendeleo ya mwaka 2025 na Mpango Mkakati wa Lishe wa Kitaifa 2016/17 – 2020/21 (NMNAP).

Amesema kuwa Halmashauri ndiyo kitovu cha utekelezaji hapa nchini na ili waweze  kukabiliana na utapiamlo inatakiwa wawe na mikakati na mipango thabiti yenye lengo hilo. .

Aidha, amesema ipo haja ya kuweza kutoa  rasilimali fedha na watu, au kwa maana nyingine kuwekeza  katika lishe.

Hivyo amesisitiza  kuhimizana katika kuhakikisha  Shilingi 1,000 ambazo Halmashauri zilielekezwa kutenga kwenye bajeti kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya kuboresha lishe kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano, zinatolewa na kutumika kikamilifu kama ilivyopangwa.

Vile vile, amewataka  kila mdau wa lishe katika Mkoa wa Dar es Salaam  aonyeshe bayana mchango wake katika kukabiliana na utapiamlo katika eneo anakotekeleza majukumu yake; sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Lishe.

Katika hitimisho la  Mkutano huo, amesema kuwa ili  kuweza kutekeleza afua za lishe kikamilifu na kuwezesha uwajibikaji na kuboresha hali ya lishe katika Mkoa wa Dar  na Taifa kwa ujumla na  kuchangia kufikia kwa malengo ya kitaifa yakujenga jamii yenye uwezo wa kubuni na yenye tija kiutekelezaji kuelekea nchi ya viwanda na uchumi wa kati.

"Panapo nia, dhamira thabiti na ushirikiano sina shaka njia itapatikana na utapiamlo utatokomea endapo kila  mmoja wetu, kwa nafasi yake ajitoe kwa dhati kuchangia katika utekelezaji wa mkataba huu wa lishe katika mkoa wetu" Amesema RAS Kunenge.

Pia amemalizia kwa kuwashukuru tena wahisani waliowezesha
kikao hiko kufanyika, pamoja   wale wote walioshiriki katika maandalizi kwa upande wa hapa Mkoani.

 Aidha,amewashukuru  wadau kwa kuitika wito huo wa kuja kwa pamoja kuwezakupanga kwa pamoja mipango na bajeti ya Lishe katika Mkoa na Halmashauri ili kuongeza kasi ya kupunguza utapiamlo na athari zake zote. Hivyo amewatakia kila la heri na mafanikio katika utekelezaji.

Naye Afisa Lishe Mkoa wa Dar es Salaam, Bib Janet Mnzava, amesema watahakikisha kila Mtoto anafikiwa na lishe bora kwa kuzingatia idadi ya watoto iliyopo ya kila wilaya huku akifafanua jinsi ya Pesa hiyo ya Shilingi 1000 itakavyotumika.

 Aidha amesema kuwa Pesa hiyo itatumika kwa Utoaji wa matunda ya Vitamini A, madini kwa wakina Mama, pamoja na utaratibu wa ufuatiliaji wa vituo vya huduma ya Afya.

Pia amesema wapo Katika mchakato wa kutembelea Shule kwa ajili ya kuwapatia Watoto wakike walio Katika umri wa kupata hedhi kwa kuwapa Madini ya chuma Katika kukabiliana na hedhi lakini lazima wawashirikishe Waalimu kwa kuwawezesha.

Amesema lengo kubwa la  Mafunzo hayo ya lishe ni kuhakikisha mipango yote ya utekelezaji wa shughuli za lishe inasimamiwa ipasavyo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.