DC MAKORI AFUNGUA KIKAO KAZI CHA WENYEVITI NA MAAFISA WATENDAJI WA SERIKALI ZA MITAA WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo mh. Kisare Makori leo amefungua kikao kazi kati ya Uongozi wa Halmashauri, wenyeviti wa serikali za mitaa na watendaji wa kata na serikali za mitaa katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Kibamba jijini Daresalaam.
Katika ufunguzi huo wa kikao hicho mh. Makori aliwashukuru wenyeviti na watendaji kwa kuitikia wito wao huo na kujitokeza kwa wingi.
Katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya aliwataka wenyeviti na watendaji kushughulikia masuala ya usafi, mapato na ulinzi shirikishi.
*"Wenyeviti na watendaji wote kwa ujumla tushirikiane kusafisha mitaa yetu, hata kwenye mapato wenyeviti tusijitoe kwa kudhani hatuhusiki na wakati sisi ndio tunaowajua wanaofanya biashara kwenye maeneo yetu"* Alisema Makori.
Mkuu wa wilaya pia aliwataka wajumbe wote wahakikishe kuna usalama wa kutosha katika mitaa yao. *"Mkahakikishe hata kile kidogo wananchi wetu wanachokitafuta na kukipata kinalindwa ili wawe na imani na serikali ya awamu ya tano"*
Mkuu wa Wilaya aliwataka wenyeviti na watendaji wakaishi kwa upendo na amani na wawe na upendo na wilaya yao ya Ubungo.
Nae Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo mh. Boniface Jacob aliuagiza Uongozi wa Manispaa kuhakikisha wenyeviti wana listi ya wafanyabiashara wanaopatikana kwenye maeneo yao. *"Wenyeviti wanaweza kusaidia kuongeza wafanyabiashara wapya kwani wao ni watu ambao wanaishi na wafanyabiashara na kuwafahamu vizuri".*
Mstahiki aliwaomba wenyeviti kutoa ushirikiano wa kutosha kwani hata Manispaa imeona umuhimu wao ndio maana ikwaita ili waweze kujadiliana baadhi ya mambo kwa maendeleo ya Halmashauri.
Mstahiki aliwashukuru wenyeviti kwa kujitokeza kwao kwa wingi na kuahidi ushirikiano wa kutosha na kukutana mara kwa mara kujadiliana juu ya changamoto za Halmashauri na namna ya kuzitatua.
Post a Comment