RC SHIGELA AWATAKA WAZAZI KUWEKEZA KATIKA ELIMU
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mh.
Martine Shigela, amewataka Wazazi na
walezi Mkoa wa Morogoro kuendelea kuwekeza katika elimu kwa manufaa ya
watoto wao na kwa maisha ya badae na Taifa kwa ujumla.
Hayo ameyazungumza Juni 01/2022 katika Mkutano wa hadhara wa
kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Kata ya Kihonda Manispaa ya Morogoro
mkutano uliofanyika eneo la Ofisi ya Kata Kihonda.
Akizungumza na Wananchi hao, RC Shigela, amesema Taifa lolote
ili liweze kupata maendeleo Wananchi wake lazima wasome na kupata elimu iliyo
bora sio bora elimu.
" Serikali yetu ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan, kipaumbele chake ni elimu na ndio maana imewekeza sana
katika Sekta ya Elimu, nawaomba wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya watoto
wenu katika sekta ya elimu na kuwalea watoto katika misingi ili wawe na maadili
waweze kufanya vizuri darasani na katika mitihani yao ya Wilaya, Mkoa na ngazi
ya Taifa na sio kuwaachia waalimu katika malezi jambo ambalo sio jema katika
misingi ya kuwalea watoto" Amesema RC Shigela.
RC
Shigela, amewataka Wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuunga mkono juhudi za
Serikali za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
juu ya Sera ya elimu bila malipo kwa kuwasomesha watoto na kufatilia maendeleo
yao kitaaluma.
"
Wanafunzi hawa ndio madaktari wa kesho na Wabunge na mawaziri tuwalinde
watoto wetu na kuwasomesha ili waweze kuwa na nidhamu" Ameongeza RC
Shigela.
Wakati
huohuo, RC Shigela, amewataka Wanawake ,Vijana na Watu Wenye Ulemavu
kuchangamkia fursa za Serikali kwa kukopa mikopo ya Serikali ambayo
inatolewa ngazi ya Halmashauri ili wafanye biashara na Kupata fedha za kulipa
ada kwa ajili ya elimu.
Hata
hivyo, amesema Mkoa wa Morogoro umepokea jumla ya shilingi Bilioni 1 kila mwezi
fedha ambazo zinaelekezwa katika Shule za Msingi na Sekondari kwa ajili ya
elimu bure bila malipo.
Mwisho,
RC Shigela, amepiga marufuku michango isiyo ya lazima shuleni huku akisema
michango yote inayotakiwa kupitishwa ipitie kwa Mkuu wa Wilaya ili iweze
kupatiwa kibali cha mchango.
Post a Comment