WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII AZINDUA TAMASHA LA UTAMADUNI, KIJIJI CHA UTAMADUNI WA KISUKUMA SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (aliyevaa tisheti nyeupe) akimkaribishaWaziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (katikati) katika Kijiji cha utamaduni wa Kisukuma alipowasili kuzindua Tamasha la Kwanza la Utamaduni Mkoa wa Shinyanga, Kijiji cha utamaduni na Filamu ya The Royal Tour kwa mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Juni 6,2022
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (aliyevaa tisheti nyeupe kushoto) akizungumza wakati Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana akizindua Tamasha la Kwanza la Utamaduni Mkoa wa Shinyanga, na Filamu ya The Royal Tour kwa mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Juni 6,2022.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amezindua Tamasha la Kwanza la Utamaduni Mkoa wa Shinyanga, Kijiji cha utamaduni cha asili na Filamu ya The Royal Tour huku akisisitiza kuwa suala la Utamaduni lazima tulipe kipaumbele katika taifa la Tanzania akisema ‘Utamaduni wetu tumerithishwa, tuwarithishe’.
Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatatu Juni 6,2022 katika Kijiji cha Utamaduni cha Butulwa – Old Shinyanga katika Manispaa ya Shinyanga ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Dkt. Chana ameupongeza Mkoa wa Shinyanga kwa kuandaa Tamasha la Kwanza la utamaduni huku akitoa agizo kwa mikoa yote kuiga mfano wa mkoa wa Shinyanga katika kujenga vijiji vya maonyesho ya utamaduni kwa ajili ya makabila yao ili kurithisha kwa vizazi vingine.
“Namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Sophia Mjema kwa ubunifu mkubwa alioufanya wa kutii na kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kila Mkoa unaenzi na kudumisha tamaduni zao hivyo Mkuu wa mkoa akaamua kufanya ubunifu mkubwa kwa kujenga Kijiji ambacho kitakuwa ni maalumu katika kuenzi na kudumisha utamaduni wa makabila yote yaliyopo katika Mkoa wa Shinyanga”, amesema Dkt. Chana.
“Shinyanga mmetia fora katika jambo hili…Ni vyema Mikoa yote nchini ikaiga mfano huu ambao umeandaliwa na Mkoa wa Shinyanga ni ubunifu mzuri mno ambao tumejionea ni kwa namna gani Machifu na Watemi zamani walivyokuwa wakiishi na maisha yao halisi pia mpangilio mzuri wa Kijiji kimoja ambacho kimekuwa na maonyesho ya tamaduni kwa wilaya zote zilizopo katika Mkoa huu hivyo nahitaji Mikoa mingine yote ifanye ubunifu huu ili tuweze kuona makabila yao na tamaduni zao zikienziwa na hili ndilo agizo la Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan”, amesema Waziri Chana.
“Mbali na kuzindua Tamasha hili la Utamaduni pia nimezindua Kijiji cha Utamaduni kwa Mkoa wa Shinyanga cha Butulwa Old Shinyanga sambamba na filamu ya The Royal Tour kwa Mkoa wa Shinyanga iliyochezwa na Rais wa Jamhuri wa Tanzania Mama Samia Suluhu yenye lengo la kutangaza Vivutio vya Utalii vilivyopo nchini pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa zaidi”,amesema Dkt. Chana.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amesema anajivunia na anaona ufahari mkubwa kwa jinsi na namna Machifu na Watemi katika Mkoa huo walivyojitoa katika kuhakikisha wanafanikisha vyema zoezi zima la kuonesha utamaduni kwa mkoa linafanikiwa vyema.
Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia kwa jinsi anavyoipeperusha vyema Bendera ya Tanzania katika kuhakikisha kila mwananchi anafurahia matunda ya nchi yake sambamba na kuitangaza nchi kimataifa.
Post a Comment