Baadhi ya shehena ya mizigo ya zao la tumbaku ikionekana katika kiwanda hicho kilichopo Mkoani Morogoro tayari kwa kuanza kazi ya uzalishaji.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro,Mhe. M,artine Shigela, amesema kufunguliwa kwa kiwanda cha Tumbaku Mkoa wa Morogoro kitatengeneza mazingira mazuri ya mzunguko wa fedha na kutoa ajira kwa wananchi.
Kauli hiyo ameitoa Juni 10/2022 alipokuwa akitembelea kiwanda hicho ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Kata zote za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro aliyoianza mwanzoni mwa wiki hii kwa ajili ya kutembelea miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Baada ya kutembelea na kuongea na Uongozi wa kiwanda hicho cha Tumbaku ,RC Shigela, amesema kiwanda hicho kilikuwa kimeajiri watu zaidi ya 3000 na wote walipoteza kazi baada ya kiwanda hicho kusimama.
Aidha, RC Shigela, ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushawishi wake wa kuwashawishi wawekezaji kuwekeza Tanzania.
"Nimefurahi sana kuona shehena ya zao hili kutoka mikoani kuanza kuingia na baadhi ya wafanyakazi kiwandani hapo wakiwa kazini, niendelee kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua nchi na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini lakini pia nampongeza sana mwekezaji mzawa wa kiwanda hiki Ndugu yangu Ahmed Huwel kwa kushawishika kuja kuendesha kiwanda hiki " Amesema RC Shigela.
RC Shigela, ametoa wito kwa wakulima wa zao la tumbaku kuanza kulima kwa wingi zao hilo kwa kuwa sasa wana uhakika wa kupeleka tumbaku yao katika kiwanda hicho ambacho kimeanza kufanya kazi.
“kwa hiyo kuna gap la tani elfu sabini ambazo kama wakulima na wananchi tuhamasike kwenda kuzalisha tumbaku kwa wingi kwa sababu tuna uhakika wa soko” Ameongeza RC Shigela.
Naye Mkurugenzi wa kampuni mpya tumbaku nchini iitwayo Amy Holdings, Ahmed Mansoor Huwel ambaye pia ni mnunuzi wa tumbaku nchini kupitia kampuni yake tanzu ya Mkwawa Leaf na mmiliki mpya wa Kampuni ya Tumbaku, ameishukuru Serikali kwa kuonesha ushirikiano na kumshawishi kuwekeza katika sekta na kutamka rasmi kuwa kiwanda sasa kimerudi nyumbani hivyo amewaomba wananchi kulima tumbaku kwa wingi na kwamba malengo yake kufikisha tani 120,000 ifikapo mwaka 2025 hivyo kutoa ajira ya kutosha kwa wananchi.
"Tumelazimika kukifungua kiwanda cha TTPL kilichopo Morogoro ambacho kilikuwa kimefungwa kwa miaka mitatu, na tumefanya hivyo ili kunusuru wakulima wetu hasa baada ya serikali kutuomba tufanye hivyo," alisema.
Kuhusu utunzaji wa Mazingira, Huwel alisema kampuni yake kwa kuanzia na kwa hali ya dharula, kwa kushirikiana na serikali, Torita na wadau wa tumbaku, itawekeza kwenye tafiti ya udongo kwenye maeneo yote nchini yanayolima tumbaku.
"Tutashirikiana na Torita ili kubaini vionjo halisi vya pembejeo maalum ya tumbaku tofauti ya hali ilivyo sasa, ambapo nchi nzima inatumia aina na idadi ile ile mifuko ya mbolea ya NPK/UREA kwa miaka zaidi ya kumi sasa huku mazingira ya udongo ni tofauti na yanazidi kubadilika," Amesema Huwel.
Aliongeza kuwa kwa pamoja watafanya kazi bega kwa bega na wakulima kupitimia mfumo wa ushirika na Bodi ya Tumbaku ili kusukuma juhudi za serikali za kubadilisha mabani ya zamani ya kukaushia tumbaku yanayotumia nishati ya miti kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na mabani ya kisasa.
Alisema kwa kufanya hivyo nchi itaweza kuzalisha tumbaku bora na sio bora tumbaku inayoendana na viwango vya kimataifa yaani compliant crop.
Alisema kampuni yake kwa kuanzia itaajiri wafanyakazi wa kuajiriwa wasiopungua 900 na huku wale wa msimu ambao mara nyingi hufanya kazi viwandani watakuwa kati ya 3000 hadi 5000 kutegemeana na msimu ulivyo.
Kampuni ya kitanzania Amy holdings imenunua mali zote za kampuni ya kimarekani Tanzania Leaf Tobacco Company(TLTC) kikiwemo kiwanda cha tumbaku cha Tanzania Tobacco Processors Limited (TTPL).
Kampuni ya TLTC ilifunga biashara zake hapa nchini miaka mitatu iliyopita na hivyo kuwarejesha majumbani zaidi ya wafanyakazi 600, athari ambayo pia iliwakumba maelfu ya wakulima na familia zao ambao walikosa soko la tumbaku yao huku maelfu ya watu wengine kwenye mnyororo huo wa thamani wa zao hilo wakiathirika.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mhe. Hussein Bashe kuwa Waziri wa Kilimo kwa kuwa amesema ni kiongozi mahili kiutendaji na mfuatiliaji wa mambo.
Aidha, amemshukuru Waziri Bashe kwa jitihada zake ambazo alianza kuzifanya tangua akiwa Naibu Waziri katika Serikali ya awamu ya tano kwa kuhangaika kukirudisha kiwanda hicho hadi jitihada zake kuzaa matunda akiwa Waziri katika ya Serikali ya awamu ya sita, na kwamba jitihada zake zinakwenda kuwakomboa kiuchumi wananchi zaidi ya 5,000 pamoja na familia zao waliaokuwa wameachishwa kazi wakati kiwanda hicho kimesimama.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando ambaye kiwanda hicho kipo katika eneo lake ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa uongozi wa kiwanda hicho na kwamba hayuko tayari kuona kiwanda hicho kinasimama tena kwa changamoto zozote ambazo zitakuwa ndani ya uwezo wake.
Post a Comment