RC SHIGELA APONGEZA MANISPAA YA MOROGORO KUPATA HATI SAFI MWAKA FEDHA 2021/2022.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe.Martine Shigela, ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na wadau wa Manispaa kwa kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni Miaka saba mfululizo kutokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Pongezi hizo amezitoa leo Juni 20/2022 katika Mkutano wa Baraza la kupitia taarifa ya utekelezaji wa Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2020/2021 katika Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro
“Hii inaonyesha Baraza la Madiwani, Mkurugenzi kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi CCM Pamoja na wataalamu wote wa Manispaa mnafanya kazi kwa kujituma na kufuata vigezo na malengo mliyojiwekea.”Amesema RC Shigela.
RC Shigela, amesema Miradi ya maendeleo ambayo imeanza na kuendelea imaliziwe na huduma kwa wananchi ziendelee kutolewa kwa viwango ili wananchi wazidi kuipenda serikali na kuchangia mapato kwa huduma bora wanazozipata.
Aidha, RC Shigela, amesema kipimo cha watumishi ni jinsi ambavyo tunaweza kusimamia utekelezaji wa Miradi yetu ya Maendeleo, hivyo amewaomba watumishi kufanya kazi kwa badii kusimamia miradi ya maendeleo na kuibua vianzia vipya vya mapato.
Hata hivyo, RC Shigela, ameipongeza Serikali kwa hatua ya kuipa Bajeti yote ofisi ya CAG kama walivyoomba kwani itaongeza ufanisi kwa ngazi ya Taifa na hata kwa Wilaya kwani wakaguzI wa ndani watakuwa na wigo mpana wa kukagua matumizi ya fedha pamoja na majengo ya serikali.
Mwisho, RC Shigela, ameiagiza Manispaa ya Morogoro pamoja Halmashauri zote kutengeneza mazingira ya kutoa elimu ya Uchumi kwa Madiwani ili waweze kuibua vyanzo vipya vya Mapato ,kuviendesha pamoja na kutafuta masoko kutoka sehemu mbalimbali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, ameipongeza Manispaa ya Morogoro kwakuwa na hati safi inayoridhisha kwa takribani miaka saba mfululizo.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando kwa kusimamia mapato na kudhibiti upotevu wa mapato.
Lengo la Baraza maalum hilo lilikuwa ni kujadili hoja mbalimbali kutoka katika Ofisi ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali pamoja na kufanyia kazi mapendekezo yaliopendekezwa na ofisi ya CAG.
Ikumbukwe kuwa, Jukumu la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa fedha za Serikali ni kukagua fedha zote za Serikali Kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, 1977 (kama ilivyorejewa 2005) na kifungu cha 45 na 48(1) cha Sheria ya Fedha za Serikali za mitaa No 9 ya 1982 (kama ilivyorejewa 2000) pamoja na kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Ukaguzi No 11 ya mwaka 2008.
Post a Comment