RC SHIGELA ATOA MIEZI 6 KUKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA UTAWALA MLIMBA.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mlimba Wilaya ya Kilombero Mkoani humo, kukamilisha ujenzi wa jengo la Utawala wa Halmashauri hiyo kabla au ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
RC Shigela, ametoa agizo hilo Juni 16 mwaka huu alipotembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo ukiwemo mradi huo wa jengo la Utawala ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi wa Wilaya zote aliyoianza Juni 12 mwaka huu.
Aidha, RC Shigela, amesema kwa sasa changamoto ya uwepo wa mvua iliyokuwepo siku za nyuma imekwisha hivyo mkandarasi anatakiwa kufanya kazi yake usiku na mchana na uongozi wa halmashauri ukisimamiwa na wahe. Madiwani uhakikishe ujenzi huo unakamilika ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
“Kile kisingizio cha mvua sasa imekwishakatika, hakikisheni mnakamilisha mradi huu kwa wakati” Ameagiza RC Shigela.
“tunataka ifikapo Disemba mwaka huu tulionao watu wote na wafanyakazi waweze kuhamia hapa na huduma zote ziweze kutolewa hapa “Amesisitiza RC Shigela.
Katika hatua nyingine, RC Shigela, ameagiza eneo ambapo jengo hilo linajengwa kulifanya kuwa eneo la taasisi za kiserikali zikiwemo Mahakama Kituo cha Polisi, TARURA, Magereza Ofisi ya DC, pamoja na Ofisi za vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama lengo ni kumrahisishia mwananchi kupata huduma za kijamii kiurahisi zaidi.
Sambamba na maagizo ,RC Shigela,ameonekana kufurahishwa sana na mabadiliko na utendaji kazi mzuri wa Halmashauri hiyo ya Mlimba kwa kufanya kazi zake kwa ufanisi na kwa mipango madhubuti lakini pia kwa kutekeleza kwa wakati maagizo kemkem ya Serikali.
Kwa sababu hiyo,RC Shigela amewapongeza Madiwani wote wa Halmashauri hiyo akiwemo Mhe. Mbunge, Mkuu wa Wilaya, Kamati yake Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo akiongoza wataalamu wake wote kwa kuonesha ushirikiano wanao kwenda nao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa pesa Jumla ya shilingi 2.8 Bil. Kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la utawala pekee huku akiahidi kuendelea kusimamia matumizi ya fedha hizo ili yaendane na uhalisia wa kazi (Value for Money).
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Innocent Mwangasa.yeye amebainisha kuwa hawana mgogoro wowote na Mkandarasi anatekeleza mradi huo katika kutekeleza majuskumu yake na kwamba anafanya kazi yake kikamilifu huku akimtaka aendelee na uzalendo huo kwa maslahi mapana ya Watanzania.
Mradi wa Ujenzi wa Jengo la utawala una gharama ya jumla ya shilingi 2.8 ambazo zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Suluhu Hassan na ulinaza Juni 2021 na ulitakiwa kukamilika mwezi Juni 30 mwaka huu na umechelewa kukamilika kwa sababu ya changamoto ya mvua na sasa mkandarasi anatakiwa kukamilisha kazi hiyo Disemba mwaka huu.
Post a Comment