Header Ads

WADAI FIDIA VIWANJA 3000 MANISPAA YA MOROGORO KUHAKIKIWA UPYA.


MANISPAA ya Morogoro ipo mbioni kufanya zoezi la kuhakiki upya wananchi wanaodai fidia ya Viwanja 3000.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 20/2022 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Mhe. Martine Shigela, katika Mkutano wa kupitia taarifa ya utekelezaji wa Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2020/2021 katika Ukumbi wa Kilakala  Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.

Akizungumza katika Mkutano huo, RC Shigela, ameitaka Manispaa ya Morogoro kuunda kamati ndogo ya kufuatilia wadai wa fidia ili kujiridhisha na kupata uhakika wa idadi hiyo kama ya kweli au la.

"Nimeona hili niliseme, tunazungumzia tuu viwanja 3000 lakini je watu hao wapo kweli? sasa niagize Manispaa undeni kamati ndogo ikishirikisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na baadhi ya Madiwani kamati ya Mipango Miji mjiridhishe hiyo idadi ya wadai ipo sawa au la, tukikuta imepungua itakuwa ni faida kwetu na tunaweza kupata nyongeza nyengine ya viwanja tukaviuza" Amesema RC Shigela.

RC Shigela, amesema viongozi kutokuwa waaminifu ndio sababu iliyopelekea kuwa na madeni makubwa ya Viwanja vya fidia, hivyo amewataka Viongozi kusimamia kikamilifu sheria ya mipango miji ili kusiendelee kujitokeza makosa kama hayo.

" Leo tuna Viwanja 6500 sisi Manispaa, lakini tunadeni la Viwanja 3000, hapa kama tungekuwa hatuna deni na tungeuza hivyo viwanja 3000 kwa makadirio ya chini ya kila kiwanja 1,000,000/= tungekuwa na Bilioni 3, sasa angalieni fedha hizi tumezipoteza kwa ajili ya uzembe na kuwa na viongozi wasio waaminifu, hili lisijirudie tena katika Mkoa huu wa Morogoro" Ameongeza RC Shigela.

Upande wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amesema atasimamia zoezi hili kikamilifu la kuhakikisha wale wadai wote wa fidia wanatambulika na wanapata haki zao.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro ,Mhe. Pascal Kihanga, amepongeza hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa na kuahidi kushiriki kikamilifu kuhakikisha zoezi hilo linazaa matunda na kufanikiwa kwa asilimia 100.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Ally Machela, amesema kati ya hekari hizo 4500, katika utekelezaji wake , Manispaa ya Morogoro itapata asilimia 45% ya viwanja vitakavyozalishwa na asilimia 55% itabaki kwa Wananchi wa eneo la Star City.

Machela, amesema  fedha zitakazopatikana kama faida baada ya kuuza viwanja  zitaiwezesha Halmashauri kuendeleza shughuli za upangaji , upimaji na umilikishaji wa viwanja katika maeneo mengine ya mji.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.