Header Ads

WAZIRI DKT. GWAJIMA APATA TUZO YA HESHIMA MOROGORO.











WAZIRI  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum Dkt Dorothy Gwajima amepokea Tuzo ya Heshma kwa kutambua mchango wake katika vita dhidi ya ukatili kwenye jamii akiwa ni Waziri mwenye dhamana.

Tuzo hiyo imetolewa na Jukwaa la "Ladies Talk Tanzania" tarehe 25 Juni, 2022 mkoani Morogoro sanjari na tuzo ya heshima kwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Martine Shigela kwakuwa Mstari wa mbele katika Maendeleo na Mazingira.

Akizungumza kwenye Hafla hiyo, Waziri Dkt.  Gwajima, amesema, anaheshimu na kuthamini Tuzo hiyo aliyopewa ambapo  kwake imekuwa chachu ya kutimiza majukumu yake, hivyo akaahidi kuendelea kutekeleza Majukumu aliyonayo bila kuchoka  ili kuitendea haki Tuzo hiyo aliyopewa.

Waziri Dkt. Gwajima amewapongeza waandaaji Wakiongozwa na Salome Sengo ambaye ndiye  Mkurugenzi Wa Ladies Talk Tanzania  kutokana na jitihada wanazochukua katika kumuinua Mtoto wa kike.

'Mmenishangaza sana, kusikia wengi wenu ni Wasomi lakini pamoja na kuendelea na Masomo bado mmejikita katika ujasiriamali unao wafanya kuweza kujikimu kimaisha lakini pia kuwasaidia ndugu zenu kwa baadhi yenu, sisi enzi zetu tukisoma tulitegemea mahitaji kutoka kwa wazazi, kwenu kizazi cha sasa ni tofauti hongereni sana" alisema Dkt Gwajima. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigella akizungumza wakati wa hafla hiyo amesema, awali kabla ya kuanzishwa kwa Wizara hiyo ilionekana kama hakuna uhitaji wake kutokana na kujumishwa kwenye Wizara ya Afya na Mambo mengi kumezwa na Upande wa Afya lakini toka imeanzishwa mambo yamekuwa ni tofauti.

"Mhe. Waziri kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Morogoro nikupongeze sana kwa kazi  kubwa unayoifanya, hivi sasa kila mmoja anatamani kuwa sehemu ya Wizara hii kwa namna wewe na Wasaidizi wako mnavyotenda kazi, Wizara inaonekana hapo ndipo unapo baini Mhe.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa na maono Makubwa katika uanzishwaji wake na Kukuteua wewe kuwa Waziri Mwenye dhamana "Alisema Mhe. Shigella.

Kwa upande wake Mkurugenzi na Muandaaji wa Tuzo hizo Salome Sengo, amesema Wanatambua na kuheshimu mchango unaotolewa na viongozi hao katika nafasi zao kwenye kusukuma gurudumu la maendeleo.

Usiku wa Ledies Talk, Umefanyika kwa Mara ya Nne Mjini Morogoro na kuwaleta zaidi ya Mabinti 175 wenye Umri kati ya miaka 15 hadi 35 ambapo wamejadiliana juu  fursa mbali mbali za kujikwamua kiuchumi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.