MANISPAA YA MOROGORO YAZINDUA MASHINDANO UMITASHUMTA.
MANISPAA ya Morogoro imezindua rasmi
mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania
(UMITASHUMTA).
Uzinduzi huo umefanyika Juni 10, 2022 kwenye viwanja vya
shule ya Sekondari Lupanga kata ya Kilakala kwa kuwashirikisha wanamichezo
kutoka shule zote za Msingi ndani ya Manispaa hiyo na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa vyama vya michezo pamoja na walimu kutoka shule hizo.
Akifungua mashindano hayo ,Justine Mkurya, ambaye ni Mgeni rasmi wa uzinduzi huo akimwakilisha Mkurugenzi wa manispaa ya Morogoro, amesema kuwa lengo kubwa la mashindano hayo ni kuunda timu kubwa ya halmashauri itakayowezesha kuleta ushindani.
“leo ndio
tunafungua rasmi mashindano haya na lengo kubwa la mashindano hayo ni kuunda
timu kubwa na bora katika halmashauri yetu kwenye michezo yote kwahiyo ombi
langu kwenu, kila mmoja ashiriki kikamilifu katika eneo alilopangiwa ili tuweze
kupata timu bora ya Manispaa ambayo itaenda kutuwakilisha vizuri kwenye
mashindano ya Mkoa ambayo mwaka huu Kimkoa yatafanyika ndani ya eneo letu hivyo
msituangushe” Amesema Mkurya
Aidha,Mkurya, amewaasa
walimu waliopewa dhamana ya kuunda timu ya manispaa kuacha kuchagua wanamichezo kwa upendeleo
“Niwasihi
walimu mliopewa dhamana ya kuunda timu ya Manispaa kuacha tabia ya kuchukua
wanamichezo kwa upendeleo, undeni timu kadri mwanafunzi mwenyewe anavyoonesha
kipaji chake katika michezo, ili tupate timu imara katika fani zote na tuweze
kushiriki kimkoa na hata kitaifa” Ameongeza Mkurya.
Pia
wanamichezo hao ambao ni wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Msingi ndani ya
manispaa hiyo wametakiwa kuhakikisha
kwamba wanakuwa na nidhamu na kujituma katika eneo walilopangiwa katika kipindi
chote cha michuano hiyo ili wawe miongoni mwa watakao unda timu ya Manispaa
badae kimkoa na kufika kitaifa.
Kwa upande wa Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro, Asteria Mwang'mbe, amewataka Waalimu wa michezo Manispaa ya Morogoro kutumia michezo ya UMITASHUMTA kuibua vipaji kupitia hazina ya Vijana wadogo waliopo katika shule za Msingi wenye uwezo mkubwa katika michezo mbalimbali.
Post a Comment