Header Ads

KAGAMBO AWAASA WAMILIKI WA VITUO VYA MAKUZI NA MALEZI WA WATOTO KUVISAJILI


Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Morogoro, Hamisa Kagambo,akizungumza na Wamiliki wa Vituo.

Mwenyekiti wa  umoja  wa wamiliki  wa day care centers -Manispaa ya Morogoroa (UWADAMO), Clarence Burchard Mkwama ambaye ndiye mmiliki wa Mary Children Day Care Sabasaba,akizungumza na Wamiliki katika Mkutano.
Katibu wa UWADAMO, Bi. Mary Kessy,ambaye ndiye mmiliki wa St.Maria Consolata SUA,akizungumza na Wamiliki wa Vituo.

KATIKA kuhakikisha watoto wanapata huduma za malezi, Makuzi na Maendeleo  ya awali kadiri ya  taratibu za serikali , Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Morogoro, Hamisa Kagambo,amewataka Wamiliki kukamilisha taratibu za usajili ili Vituo hivyo visajiliwe.

Akizungumza na wamiliki wa vituo vya makuzi na malezi kwa watoto wachanga na watoto wadogo,Kagambo, amesema kikao cha leo Juni 29/2022, kina lengo la kusaidia uboreshaji wa  huduma kwa watoto  vituoni ikiwepo  wamiliki kuendelea kufanya  usajili wa vituo, kwani kwa  kufanya hivyo kunaongezea thamani vituo hivyo na kuvifanya  vitambulike  rasmi  kisheria.

Kagambo amesema, watoto kuwepo  katika vituo  hivyo kunasaidia ulinzi na usalama wa watoto, kuwepo kwa ujifunzaji wa awali kwa  watoto na wazazi /walezi wanapata muda wa kufanya shughuli  za kiuchumi.

Akizungumzia kuhusu serikali imejipangaje kuhusiana na huduma vituoni, Kagambo,  amewaasa wamiliki wa vituo vya Malezi na makuzi kuvisajili Serikalini ili watambulike na shughuli zao zitambulike Serikalini.

Amesema usajili wa vituo hivyo ni bure kwani sheria ya mtoto namba 21 ya Mwaka 2009 kifungu cha 147 mpaka 152 na kanuni za watoto imetoa ufafanuai kuhusu vituo vya kulelea watoto wadogo na watoto  wachanga  mchana na  imeeleza taratibu za kufuata wakati wa kufungua vituo vya makuzi na malezi kuwa na vigezo vinavyohitajika.

" Manispaa ya Morogoro tuna jumla ya vituo 103  vinavyojulikana na ustawi wa jamii kati ya hivyo vimesajiliwa vituo 25 na vituo 5 vipo katika mchakato , hivyo  ni  vema kwa kila  anaeanzisha vituo avisajili kwanza  kwaajili  ya kumlinda mtoto" Amesema Kagambo.

Naye, Mwenyekiti wa  umoja  wa wamiliki  wa day care centers -Manispaa ya Morogoroa (UWADAMO), Clarence Burchard Mkwama ambaye ndiye mmiliki wa Mary Children Day Care Sabasaba, ameipongeza Ustawi kwa kusimamia UWADAMO na kuepelekea kuongeza  uelewa kwao na kuanza kufanya  mabadiliko  chanya  ya kutoa  huduma  za vituo   kwa watoto na kuwepo  na umoja  huo utawasaidia  kujadiliana na kupeana uzoefu  katika eneo la huduma vituoni.

Upande wa Katibu wa UWADAMO, Bi. Mary Kessy,ambaye ndiye mmiliki wa St.Maria Consolata SUA, amesema  serikali  na wadau wasichoke waendelee na jitihada hizo na ikiwezekana kutoa mafunzo hadi  kwa wazazi/walezi yawafikie ingawaje  pia wao  kama wamiliki  na walezi vituoni watasaidia kutoa  elimu  ya malezi kwa wazazi/ walezi katika vituo.

Kwa upande wa Mwakilishi wa wamiliki kutoka Hittler Day Care , ameushukuru Uongozi wa UWADAMO, kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro katika kutoa elimu na kupelekea  kusaidia uundaji wa umoja  wa wamiliki  wa day care centers -Manispaa ya Morogoro ambapo Umoja huo umekuwa msaada wa  kuongeza  ujuzi kwa wamiliki  na walezi.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.