Wananchi wa Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika uchangiaji wa shughuli za maendeleo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akizungumza na kusalimiana na Wananchi waliofika katika ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarsa Shule ya Msingi Nane Nane Kata ya Tungi uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare katika ziara yake ya kukagua miradi ya Maendeleo Kata ya Tungi
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Maziwa Shamba Milk kilichopo Kata ya Tungi mara baada ya kutembelea Kiwanda hicho.
Zahanati ya Kata ya Tungi ikiendelea na Ujenzi ,ambapo Shilingi Milioni 9 na laki 7 zimetoka Serikali Kuu na Shilingi Milioni 17 zimetolewa na Manispaa ya Morogoro. |
Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John (katikati) akiteta jambo na Afisa Tarafa Manispaa ya Morogoro . (kulia) Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba. |
Watumishi wa Manispaa ya Morogoro wakifuatilia kwa umakini hotuba ya Mkuu wa Mkoa katika Kiwanda cha Maziwa cha Shamba Milk. |
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga akihotubia Wananchi katika Shule ya Msingi Nane Nane iliyopo Kata ya Tungi. |
Hayo yamezungumzwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Sanare , katika muendelezo wake wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kujua kero za wananchi katika Kata ya Tungi leo Machi 3,2020.
Akizungumza na Wananchi wa Kata ya Tungi, RC Sanare, amesema uhamasishaji wa kuchangia Miradi ya maendeleo hususani katika elimu, Miundombinu, afya na mengineyo ni jambo jema katika kuunga mkono juhudi za serikali zinazofanywa katika eneo lao.
RC Sanare , amesema katika miradi yoyote ya maendeleo jambo la kwanza linalotakiwa kufanyika ni kuona nguvu ya Wananchi inatumika harafu Serikali wao wanamalizia.
Ametolea mfano wa Shule ya Msingi, Nane Nane iliyopo Kata ya Tungi ina wanafunzi wapatao 2113 lakini changamoto iliyopo ni ukosefu wa madarasa 47 ambapo kwa sasa shule hiyo ina jumla ya madarasa 11 hivyo ili kufikia maendeleo ni lazima wananchi wachangie na Serikali kuona wapi wamekwama kwa vile miradi hiyo ni ya wananchi na siyo ya Serikali.
Amesema kwa mujibu wa sheria na taratibu kila darasa moja wanatakiwa kukaa wanafunzi wasiopungua 45.
Amesema darasa moja kukusanya wanafunzi kupita kiasi ni sawa na Mkutano wa Wanafunzi na hata uelewa wao ni mdogo ukilinganisha na darasa lenye watu wachache jambo ambalo linapekea kushuka kwa viwango vya elimu.
'Nitoe agizo kwa Afisa Utumishi, Afisa Tarafa pamoja na Watendaji wa Kata hii na wenye Viti wa Mitaa yote 12 katika Kata ya Tungi mkae chini muangalie ni kwa namna gani mnaweza kuweka mipango ili kuongeza madarasa yaliyopungufu na watoto wetu wakasoma vizuri na kufaulu, hali ni mbaya tusiwalaumu tuu wananchi hachangii lakini nyie viongozi lazima muonyeshe njia na mkazo na muwaambie ukweli wazazi wachangie , tukifanya hivyo shule zetu zitapendeza na tutapata matokeo mazuri, hatutaki shule yenye mrundikano wa Watoto tunataka shule zenye kutoa elimu bora"Amesema RC Sanare.
Katika Ujenzi wa Zahanati ya Tungi, RC Sanare ,amewataka watendaji kukaa na wananchi katika Zahanati hiyo kufanya vikao na kuona jinsi ya kuweza kuchangia fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo hilo ili liweze kutoa huduma kwa wananchi na kupunguza adha zinazowakumba kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya afya.
"Mna bahati sana wananchi wa hapa mmepata bahati ya kuletewa fedha za kutekeleza miradi ya ujenzi hususani huu wa Zahanati ya Kisasa lakini kasi ya wananchi katika kuchangia ni ndogo sana kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Serikali kumbukeni kuwa kwa kufanya hivyo ni kuvidhulumu vizazi vyenu viliyopo na vijavyo,taarifa niliyonayo ni kwamba wananchi wamechangia laki 7 tu , bado haitoshi ongezeni nguvu, Watendaji kaeni na watu wenu muwaeleze namna ya kuchangia hapa, isijetokea kiongozi akawarubuni na kuwapiga kiswahili kwamba msichangie, maendeleo hayana chama iwe CCM, CHADEMA , CUF na Vyama vyengine wote mtatibiwa , kikubwa msiyumbishwe na wanasiasa Uchwara wasio kuwa na wivu wa maendeleo kazi kutaka kujilimbikizia wenyewe na kuingiza Siasa katika masuala muhimu kwa wananchi" Amesisitizia RC Sanare.
RC Sanare amesema kuwa sekta ya elimu ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya nchi ambapo inabidi juhudi zaidi ziongezeke kuweza kuifanya elimu kuwa silaha bora itakayowasiadia vijana kuondokana na umaskini.
“Nataka kueleza na hili ili mulielewe, Mzazi unaweza kumwachia kijana wako mali, lakini itakwisha, ukimwachia elimu hakika huu ndiyo urithi pekee watanzania wenzangu, tujitoe kuchangia sekta ya elimu kama ambavyo tunafanya katika sherehe na kumbuka maisha ya sasa bila elimu utasababisha mwanao awe katika maisha magumu hapo mbeleni hivyo tusisubiri serikali tuwe na utamaduni wa kuchangia katika sekta hii ya elimu ndugu zangu,” Ameongeza RC Sanare.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amesema kuwa katika maeneo yote aliyopita yenye miradi ya ujenzi wa madarasa wananchi wanatakiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ili kuwatia moyo viongozi na kuendelea kuwapelekea miradi mengine.
"Kama wananchi mtashindwa kushiriki katika uchangiaji wa maendeleo katika ujenzi wa miradi inayowahusu , kiukweli jambo hilo litapelekea kuwavunja moyo viongozi kuendelea kuwapelekea miradi jambo ambalo litawaumiza wananchi, kikubwa kaeni katika viako vyenu vya maendeleo mkishapitisha nileteeni ili tuone na namna ya kuwapatia vibali vya michango muendelee na majukumu ya ujenzi wa miradi na kuonesha angalau katika miradi fulani nguvu za wananchi zimeonekana kuliko kila kitu kuwaachia Serikali ile hali miradi ni ya kwenu Wananchi" Amesema DC Chonjo.
Ameenda mbali zaidi na kuwataka Wananchi kushiriki Mikutano inayoitishwa na Viongozi wao kuanzia ngazi za Mitaa, ili wachangie mawazo yao katika masuala ya Maendeleo.
Hata hivyo, DC Chonjo, amewataka Watendaji wa Kata Manispaa ya Morogoro, kuwa chachu katika kuhamasisha shughuli za kimaendeleo na kuwa wavumilivu ili kuwapa nafasi Viongozi waliokuwa Madarakani kutekeleza yale yaliyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi CCM ya Mwaka 2015.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, mhe. Pascal Kihanga, ameendelea kuwaeleza kuwa wanapochangia maendeleo na kuboresha miundombinu ndipo wanapoongeza pia kiwango cha ufaulu kwani wanafunzi wanakuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia na walimu mazingira mazuri ya kufundishia.
Meya Kihanga, amesema kuwa urithi pekee kwa watoto ni elimu hivyo ni jukumu la wazazi kuchangia sekta ya elimu kuliko kusubiri serikali ambayo ina mzigo mkubwa kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo katika kukuza uwezo wa wanafunzi katika mambo ya masomo.
"Ndugu zangu elimu bila malipo haiondoi wajibu wako kama mzazi, haiondoi wajibu wako kama jamii hivyo ni lazima tuchangie shughuli za maendeleo ili kusaidia watoto wetu tusiachie Serikali kila kitu, Kila mmoja anawajibu wake, Kamati za shule zinawajibu wake na bodi za shule zina wajibu wake "Amesisitizia Meya Kihanga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mnaispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewasihi wananchi wa Manispaa ya Morogoro hususani wa Kata ya Tungi ambapo ziara imefanyika leo kuwa na uchungu na maendeleo ya eneo lao na kuachana na migogoro isiyokuwa na tija kwani inawapotezea muda wa kufanya shughuli za maendeleo.
Aidha, Sheilla, amewataka wananchi wa kata ya Tungi kutokatishwa tama wanapojitoa kufanikisha shughuli za maendeleo sanjari kuwaunga mkono viongozi wao waliowachagua.
Mkazi wa Kata ya Tungi, Ayubu Mohamed, ameushukuru Uongozi wa Mkoa, Wilaya na Manispaa kwa ziara hizo huku akiamini ni moja ya njia ya kuwapelekea maendeleo na kuwataka Viongozi wasisite kufanya ziara kama hizo zenye malengo makubwa ya kutatua kero za wananchi wanyonge wenye matumani na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli.
Post a Comment