Header Ads

Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro awalima faini waliokiuka bei elekezi ya Vitakasa Mikono vya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA .

Miongoni mwa Duka la Dawa la SHIV PHARMACEUTICAL LTD lililopo Mtaa wa Old Dar Street jirani na Kituo cha Dalala Mjini lililopigwa faini na kufungiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kufuatia  kukiuka agizo kwa kuuza Vitakasa mikono (Sanitizer ) kwa bei ya juu tofauti na bei elekezi inavyotaka. 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akimtaka mmoja wa wahusika wa Mabasi (mbele yake) kulipa faini baada ya Basi lake kushindwa kuweka Kitakasa Mikono kwa abiria wake ili kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akizungumza na Dereva wa Bajaji na kumtaka amuonyeshe Kitakasa mikono alichoweka katika Bajaji yake. (kushoto) Maganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Ikaji Rashid. 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akitoa elimu na maagizo kwa wasafiri pamoja na Madereva wa Mabasi na Noa katika Stendi ya Mabasi Msamvu ili kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba (kushoto) , akimuunga mkono Mjasiriamali anayefanya shughuli zake Stendi ya Mabasi Msamvu.


Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr Ikaji Rashid (kulia) akitoa maelekezo kwa Konda wa Mabasi Stendi ya Msamvu.
Kondakta wa Basi la Kampuni ya New Force, akimnawisha abiria wake kabla ya kupanda Basi.
Baadhi ya abiria wakinyunyiziwa dawa ya Vitakasa Mikono kabla ya kupanda gari.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,Msimamizi wa New Shani Sinema Pub & Restaurant (kushoto kwa Mkurugenzi), Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Ikaji Rashid (katikati) pamoja na Afisa Biashara Manispaa ya Morogoro, Festus Herman wakipata maelekezo baada ya kuifungia Bar hiyo kwa kosa la kukutwa  mifereji ya bar hiyo ikitiririsha maji machafu.



MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amewapiga faini na kuvifungia vituo vinavyouza bei ya Vitakasa mikono kwa gharama kubwa tofauti na bei elekezi ya Serikali.

Hayo yamejiri leo Machi 24, 2020, kufuatia agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa la kuwataka wale wote wanaouza vitakasa mikono tofauti na bei elekezi kushughulikiwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Sheilla, amesema kitendo cha kuwapiga faini ni moja ya njia na fundisho sahihi kwa wale wanaoendelea wanaouza na kupandisha bei  juu ya Vitakasa Mikono kwa kujipatia faida zaidi na kwenda kinyume na matamko ya Viongozi wa Ngazi za juu.

Amesema kuwa suala la Ugonjwa wa CORONA wafanyabiashara wasiichukulie kuwa ndio njia ya kujipatia vipato badala yake wafuate utaratibu wa bei elekezi ambayo Serikali imeweka kutoka kwa Mamlaka husika ya MSD.

“Tumeanza kuchukua hatua, hii iwe fundisho kwa wale wanaoenda kinyume na Sheria , tayari Viongozi wetu washatoa matamko na maangalizo juu ya kupandisha bei kiholela vifaa vya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA lakini cha kushangaza bado wapo watu ambao sio Wazalendo wanafanya Biashara ya kukomoana katika majanga haya. , leo nimeingia mwenyewe hapa dukani  Shiv Pharmaceutical Ltd  nikanunua Sanitizer Shilingi 4000 yenye Mills 100 wakti inauzwa Shilingi 2000,  haiwezekani wenzetu huko wanakufa kwa Ugonjwa huu lakini nyie badala kuwasaidia Watanzania wenzenu ndio kwanza mnawakandamiza mnafikiri bei mtakayo weka ni wote wataimudu? Nitoe rai kwa mfanyabiashara yeyote ndani ya Manispaa yangu akienda kinyume na Serikali nitamshughulikia na ikiwezekana kumfutia hata leseni tusicheze mchezo na maisha ya watu Viongozi wanajitahidi kuhamasisha kujikinga nyie mnataka faida mwanzo mwisho tufuate sheria , kanuni na taratibu za Nchi zinavyotaka “ Amesema Sheilla.

Aidha hakuishia hapo, kwani aliendelea na Ziara yake ya kukagua Vituo vya Mabasi ikiwemo Kituo kikubwa cha Mabasi Msamvu pamoja na Vituo vidogo vya  Daladala huku akisisitizia sana kila Basi liwe na Vitakasa Mikono pamoja na Maji tiririka na sabuni ili kabla ya mteja au abiria kupanda aanze kunawa na kupuliziwa vitakasa mikono katika kujikinga na Ugonjwa wa CORONA ambapo katika wakati huo pia ameyapiga faini ya Shilingi lakini 100,000/ kwa kila Basi ambalo halina  Vitakasa Mikono kwa ajili ya abiria  .

“Nimeanza kuridhishwa nafikiri elimu sasa imewafikia lakini bado wapo wengine wanaenda kinyume, hivyo tumechukua hatua za kupiga faini Magari ambayo hayana kinga za Ugonjwa huo na kuwaonya vikali kuwapiga faini na  kuwapatia elimu zaidi ili abiria wawe salama katika safari zao, niwaombe tena Ugonjwa huu ni hatari sana Wamiliki wa Vyombo vya Moto, Bodaboda, Bajaji , Daladala, Haisi pamoja na Mabasi makubwa hakikisheni Vitakasa Mikono mnakuwa navyo kabla ya abiria kupanda safisheni magari yenu kwenye siti na sehemu zote abiria wanazoshika mnyunyize dawa na muwanyunyizie mikononi  kabla ya  abiria kupanda watakao kwenda kinyume tutawashughulikia” Ameongeza Sheilla.

Mbali na kukagua bei za Vitakasa Mikono na mabasi pia amepata nafasi ya kukagua usafi na mazingira katika Bar ambapo katika ukaguzi huo ameifungia na kuitoza faini  Bar moja  inayojulikana kwa jina la New Shani Sinema Pub & Restaurant   iliyopo Kata ya Boma Mtaa wa Old Dar Street jirani na Kituo cha Daladala Mjini inayomilikiwa na Ndg. Godwin Harrison Mkisi , na kumpa siku 2 kukamilisha usafi wa mifereji inayotiririsha maji machafu.

Naye, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Ikaji Rashid, amesema lengo la ziara hizo za mara kwa mara ni kuona utekelezaji  na maagizo kutoka kwa Viongozi wa ngazi za juu kama  unafuatwa .

Amesema pamoja na Mkurugenzi kupiga faini lakini wametoa zaidi elimu ya kutosha dhidi ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA na kuwahatadharisha kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wenye tabia ya kukiuka maagizo ya Viongozi kwa makusudi.

“Zoezi linakwenda vizuri asilimia 80 watu wameitika lakini bado wapo watu wachache ambao sio waelewa  lakini tulichokifanya ni kuwapiga faini na wale wenye maduka ya Dawa (Pharmacy) tumewachukulia Leseni zao za biashara huku tukiwataka watuonyeshe risiti za mauzo yao za vifaa vya Vitakasa mikono ikiwamo Sanitezer zenyewe, Maski ili tuone nasisi tutoe neon kuliko kila mtu kujiamulia atakavyo , lakini bado tutaendelea kupita duka kwa duka , Mtaa kwa Mtaa kuangalia wale wanaoenda kinyume na maagizo yetu, tunataka Manispaa yetu iwe salama na Ugonjwa huu, niwaombe wafanyabishara hususani wenye maduka ya Dawa kama mtaendelea na tabia hii ya kupandisha bei tutawapiga faini sana na kuwanyang’anya Leseni zenu za biashara” Amesema Dr. Ikaji.

Aidha, amesema ili kuhakikisha zoezi hilo lianfanikiwa kwa asilimia 100 tayari wameshatenga makundi  makuu 3 ambapo katika makundi hayo kundi la kwanza lianashughulika na ufuatiliaji wa bei elekezi ya dawa na Vitakasa mikono, na kundi la pili kwa ajili ya kuzunguka katika Nyumba za wageni pamoja na Hoteli zote kubwa kuangalia Vitakasa mikono pamoja na jinsi nguo wanazozitumia katika nyumba hizo zina usalama wa kiasi gani maana lazima zifuliwe kwa uamkini na kundi la mwisho na la tatu linashughulika na kutembelea  Mama na Baba lishe kwa ajili ya kutoa elimu zaidi.

Kwa upande wa Afisa Biashara Manispaa ya Morogoro, Festus Herman, amesema ni marufuku kufanya biashara kinyume na sheria hivyo kila mfanyabisahara afuate taratibu za Leseni yake jinsi inavyomruhusu kufanyabisahara nasio kujipangia bei kiholela.








No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.