MANISPAA YA MOROGORO YAUNGANA NA TASWO KUWAFARIJI NDUGU WA MAREHEMU WA AJALI YA MOTO MASAMVU.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, mhe. Pascal Kihanga, akimkabidhi kiloba cha Unga mmoja ya ndugu wa marehemu waliyopata ajali ya moto Msamvu. |
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga , akimkabidhi daftari kwa ndugu wa marehemu, (kulia), Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana. |
Add caption |
Baadhi ya ndugu Ndugu wa marehemu waliojitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani yaliyofanyika Kitaifa Manispaa ya Morogoro, Kata ya Mwembesongo. |
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga,
ameitaka Jamii itambue umuhimu wa kukuza mahusiano baina ya watu na watu ili
kuchochea ukuaji wa kiuchumi hapa nchini.
Hayo ameyazungumza leo Machi 17,2020 katika Ofisi ya Kata ya Mwembesongo wakati wa
hafla fupi ya Jumuiya ya Wataalamu wa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO) kwa
kushirikiana na Idara ya Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro walivyotembelea wajane na tegemezi wa marehemu waliofariki katika ajali ya Moto Msamvu na kuwapatia msaada wa vyakula
ikiwa ni moja ya maandalizi ya maadhimisho
ya siku ya Ustawi wa Jamii Duniani .
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mhe. Kihanga,
amekipongeza Chama hicho kwa jitihada za
kuwajali tegemezi wa marehemu kwani wamefanya jambo la kiungwana linalostahili
kuigwa na jamii kwa kuwakumbuka wajane wa wahanga wa ajali ya Moto Msamvu.
Aidha, amesema Jamii isiyokuwa na matatizo ya kijamii na migogoro
ya nafsi kwa mtu mmoja mmoja ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi katika nchi
yoyote.
“Niwapongeza sana TASWO
Taifa kwa kuwajali ndugu zetu, kwani wengi wao wameacha wajane wakiwa na
watoto hali hii imefanya familia zao ziwe tegemezi kwa kiasi Fulani, hivyo
niseme kuwa upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya ukuaji wa uchumi wanchi na
utengamano wa Kijamii kwa wananchi wa chi husika, kamwe hatuwezi kutenganisha
maendeleo ya kiuchumi ,kisiasa,
kitamaduni na Ustawi kwa jamii katika nchi kwani yote haya hutegemeana , na
tukumbuke kwamba mahali ambapo Ustawi wa kweli wa Jamii haupo hata maendeleo ya
kweli ya katika Nyanja zote huathirika na wakati mwengine kutokuwepo kabisa,
hivyo TASWO mmetushika mkono kilichobakia Manispaa Ustawi wa Jamii pamoja na
Viongozi wa Kata hii msisubirie mwaka kwa mwaka mjenge utaratibu wa
kuwatembelea hawa ndugu zetu na kuwasaidia kile mlichonacho hata kama sio pesa
hata ushauri wa nini wafanyaje itakuwa jambo la faraja sana kwao na kujisikia
wanatahminiwa ”Amesema Mhe. Kihanga.
Pia , amesema Serikali imewatambua marehemu hao hadi kufikia
kuwatengenezea uzio wao lakini na mpango uliopo kwa sasa ni kuwajengea makaburi
ya pamoja yenye kufanana na kuweka mnara mkubwa utakao kuwa na majina yao
warehemu wote ili iwe sehemu moja ya kuwakumbuka na ndugu wakiwa wanataka
kuwaona itakuwepo sehemu kwa ajili ya dua kwa dini zote.
Amesisitiza huku akisema kuwa kuwa ndugu wa marehemu wajenge utamaduni wa
kuwaombea ndugu zao mara kwa mara na sio kusubiria kila mwaka kama Serikali
ilivyojiwekea utaratibu wa kuwakumbuka.
Katika hatua nyengine, amesema maendeleo ya Ustawi wa Jamii
ni muhimu sana kama ilivyo maendeleo katika Uchumi na hasa kwa sasa ambapo
Taifa linafanya kila Jitihada ya kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati na
Viwanda ifikapo mwaka 2025, ambapo hayo yote yanaenda sambamba na kuhakikisha
uhusiano wa Watu na Ustawi wa Jamii kwa ujumla upo katika hali ya kuridhisha .
Naye Mwenyekiti wa TWASO Taifa, Dr. Mariana Makuu, amesema
katika kuunga mkono Juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano Chini ya
Rais , Mhe. Dkt. John Magufuli , kwa kutambua umuhimu wa maadhimisho hayo
wameona ni vyema wakawakumbuka wajane pamoja na tegemezi wa Marehemu
waliofariki kwa ajali ya Moto Msamvu baada ya Lori la Mafuta kushika moto.
Amesema tukio hilo
litabakia kuwa la kihistoria hivyo wao kama TWASO kwa kushirikiana na Idara ya
Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro, wameona ni vyema wakawakumbuka kwa
kuwapatia vyakula , madaftari, peni , sabuni pamoja na mafuta ya kula ili
waendelee kujikimu kimaisha katika kipindi kigumu wanachopitia.
Dr. Makuu amesema Wataalamu wa Ustawi wa Jamii wameendelea
kubaki ni kichochoeo cha kuimarisha mahusiano ya watu wote na hili wanalifanya katika maisha
yao ya kila siku ya Kitaaluma na kazi na pale inapotokea mahusiano ya watu yana
shaka au dosari basi kazi kubwa ya kufanya hafua ya kurejesha mahusiano hayo
kwa sehemu kubwa huwa ni kazi ya Wataalamu wa Ustawi wa Jamii.
“Kila Mtanzania popote alipo anayo haki ya kupata huduma
bora za Ustawi wa Jamii na kulinda Utu na heshima yake, heshima ya mtu mwingine
ikiwa ni pamja na Heshima ya Taifa kwa ujumla, ambapo ndio maana hata Ilani ya
Chama Tawala kinachoongoza Serikali yetu imeangalia kwa kina masuala ya Ustawi
wa Jamii katika Ibara zake tofauti” Amesema Dr. Makuu.
Amesema kuwa katika kuadhimisha Sikuu hiyo ya Kitaifa, TASWO
Morogoro imeona umuhimu wa kukuza mahusiano ya watoa huduma za Ustawi wa Jamii
na wapokea huduma kwa kuzitegemeza baadhi ya familia ambazo ziliwapoteza ndugu
wa karibu katika janga la mlipuko wa gari la mafuta ya Petroli lililotokea
tarehe 10 Agosti 2019.
Amesema TASWO inatanguliza shukrani kwa wale walioonyesha
utayari wa kuwaonga mkono juhudi za maadhimisho
ya Siku ya Ustawi wa Jamii Duniani (WORDL SOCIAL WORK DAY) iliyoadhimishwa
Kitaifa Manispaa ya Morogoro ambapo maadhimisho hayo hufanyika duniani kote
kila mwaka kuanzia wiki ya pili mpaka ya mwisho wa mwezi wa tatu ambapo kauli
mbiu husema ‘Umuhimu wa kukuza mahusiano
ya Watu hasa katika kuleta mabadiliko”.
Hata hivyo ametoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Manispa ya
Morogoro, NMB, CBO kwa kutoa msaada wa
kufanikisha maandalizi hayo na siku yao ya kujumuika na ndugu wa maehemu katika
kuwapatia misaada hiyo.
Kwa upande wa Afisa Ustawi
wa Jamii Manispaa ya Morogoro, Bi. Sidina Mathias, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa
Manispaa ya Morogoro, amekishukuru Chama cha TASWO kwa moyo waliouonyesha kwani
zipo sehemu nyingi zenye shida lakini wameona Manispaa ya Morogoro kuwa sehemu
moja wapo ya kufanikisha siku hiyo ya Maadhimisho ya Siku ya Ustawi wa Jamii
Duniani.
“Nawapongeza sana ndugu zetu wa TASWO ,hiki walichokionyesha
kimetufariji sana , tunaomba ushirikiano huu wa Kitaaluma uendelee ili kuleta
mafanikio chanya katika Nyanja mbalimbali hususani katika kuwasaidia watu ambao
wamekosa faraja na tegemezi katika familia, sisi kama Manispaa kwa niaba ya Mkurugenzi
wa Manispaa tunaungana kwa pamoja na hili lisiishie hapa hata katika
maadhimisho mengine tuendelee kuwakumbuka watu wenye changamoto katika jamii na
hata vile vituo vya kulelea Wazee na watu wanaoishi katika Mazingira magumu na yatima” Amesema Sidina.
Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana,
ameushukuru Ungozi wa TASWO kwa faraja walioinyesha wakishirikiana na Manispaa
ya Morogoro kwani kitendo hicho kitaamsha hali ya ndugu wa marehemu kujiamini
na kuona wana thamani sawa na watu wengine.
Lakini amewaonya wananchi wa Manispaa ya Morogoro hususani wakazi wa
Kata yake kuacha tabia ya kukimbilia vitu vyenye madhara wanapoona kuna dalaili
hizo au kuna matuko yenye madhara yametokea kwani huatarisha maisha yao.
“Nichukue nafasi hii kuwaomba tena wananchi, pale mnapoona
kuna madhara tafadhali msiyakimbilie badala yake ondoka eneo hilo haraka sana ,
tukiyakimbilia mwisho wa siku tunasababisha madhaara kama yaliyowakuta ndugu
zetu, lakini nawashukuru sana TASWO na Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro kwani zipo sehemu nyingi
za kusaidia lakini wamekuja katika Kata yangu najisikia faraja sana “ Amesema
Mhe. Kalungwana.
Post a Comment