Header Ads

DC CHONJO AIUNGA MKONO TAASISI YA WILDNA FOUNDATION KWA KUWAPA KIASI CHA SHILINGI MILIONI MOJA KWA AJILI YA KUWASAIDIA WANAWAKE WANAOISHI KATIKA NYUMBA ZA POLISI MANISPAA YA MOROGORO.



Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, (kushoto), akikabidhi  kiasi cha Shilingi Milioni Moja , kwa Mwenyekiti wa Wildna Foundation, Bi. Yustina Mutafungwa kwa ajili ya kutunisha mfuko wa kuwasaidia kujiendeleza kiuchumi kwa wakina  Mama wanaoishi katika nyumba za Polisi Manispaa ya Morogoro.  

MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ametoa kiasi cha Shilingi Milioni Moja 1,000,000/= kama ahadi aliyoiahidi kwa Taasisi ya Wildina Foundation inayojishughulisha  na kuwasaidia kuwanyanyua kiuchumi pamoja  na kuwaendeleza  wakina  Mama wanaoishi katika nyumba za Polisi Manispaa ya Morogoro  inayoongozwa na Mama Yustina Mutafungwa ambaye ni mke wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro .

Hafla hiyo fupi ya kuwakabidhi fedha hizo ikiwa ni njia ya kuwaunga mkono wakina Mama wanaoishi katika Nyumba za Polisi Manispaa ya Morogoro, imefanyika leo Machi 19, 2020 Ofisini kwake.

Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Chonjo, amesema kuwa ametoa kiasi hicho cha fedha kama ahadi yake kufuatia kuwaahidi katika mkutano walimualika  wa harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya kupata mtaji wa kuendeleza Taasisi hiyo  ikiwa na lengo la kujikwamua kiuchumi.

“Natoa fedha mimi nikiwa Mkuu wa Wilaya hii ya Morogoro,najua  Taasisi hii imekuwa msaada mkubwa kwa  wakina Mamam hapa mkoani Morogoro bila kusahau mimi pia Mwanamke mwenzao , fedha  hizi ni ahadi yangu kwenye harambee waliyonialika  , lakini natarajia kuona fedha hizi zitakwenda kutunisha mfuko wenu wa uwezeshaji wa kiuchumi wa wakina mama, natambua kwamba wakina mama ambao ni wake wa Polisi ni ndugu zetu na hawa ndio ambao wanawalinda Askari zetu wanaolinda usalama wa raia na mali zao,  kwahiyo wanapokuwa na jambo lao lazima sisi Viongozi tuwaunge mkono, maana kukiwa na maugovi na mapungufu katika Familia hata hawa askari wetu wanakosa hali ya kutulinda sisi Wananchi, tunafahamu hali zetu katika mishahara ”Amesema DC Chonjo.

Aidha amesema kitendo cha kuundawa kwa Taasisi hiyo kumetokana na  kujiongeza kwa Wakina Mama kwani wengi wao wanafamilia hivyo wameona ni vyema wakajiingiza  katika shughuli za Ujasiriamali kwa kuuza Chakula, Mapambo , Ushonaji wa Nguo, ushonaji wa Vikapu na mikeka pamoja na  kufanya shughuli nyengine ili waweze kujikomboa na kuacha utegemezi na kuzilea familia zao zikaaishi maisha bora.

Amesema kutokana na juhudi walizozionesha zilimfanya kuwaunga mkono ili waweze kufanya shughuli zao za kuongeza kipato katika Familia ukizingatia wao ni wakina Mama kama alivyo yeye na anategemea baadaye kuwaona wakiwa na maisha mazuri huku wakitembea kifua mbele.

Pi amesema kuwa hatua waliyofikia ni  madhubuti ya kujenga uwezo wa wanawake waweze kujitegemea ili waweze kufanya maamuzi juu ya maisha yao na kutekeleza maamuzi hayo kwa kutumia rasilimali zilizopo bila kuingiliwa au kubughudhiwa na mtu, taasisi au chombo chochote kwa sababu tu, wao ni wanawake.

Naye Mwenyekiti wa Wildina Foundation, Bi. Yustina Wilbrod Mutafungwa, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa upendo na moyo aliouonyesha kwa kuwakabidhi ahadi aliyoiahidi katika harambee waliyomwalika.

Amesema kuwa, mchango wake hautaenda bure, bali watautumia kwa malengo waliyokusudia ili kuweza kusongesha gurudumu mbele la kuongeza kipato katika familia za  wakina mama wanaoishi katika Kambi na nyumba za Polisi.

“Tunamshukuru sana Mama yetu Chonjo, amekuwa mstari wa mbele sana kusaidia jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi ukizingatia naye aliolewa na askari, hivyo kama Mwanamke  na Mama mwenzetu amekuwa ni  mtu wa karibu sana kwetu , kila tunapopata jambo tukimwambia amekuwa mtu wa maamuzi na kutusaidia alituahidi na leo ametekeleza lakini kwa hili la leo tutamuhakikishia kwamba tutarudi Ofisini kwake tukiwa kifua mbele kabisa kwa mafanikio tutakayoyapata kikubwa aendelee na Moyo huo huo na asituchoke pale tutakapokuwa tumekwama “Amesema Mama Mutafungwa.

Amesema lengo la kuanzisha Taasisi hiyo ni kuweza kuwanyanyua wakina Mama na wanawake wanaoishi katika Nyumba za Polisi kwani wengi wao wanaishi katika mazingira magumu na hawawezi kufanya kazi na vipato vyao ni vidogo.




No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.